Viongozi wa ECOWAS waazimia kuikabili Ebola
16 Desemba 2014Mwenyekiti ya Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS, rais wa Ghana John Mahama alisema uasi, machafuko ya kisiasa na usalama ndiyo matatizo makubwa yanayoyakabili mataifa ya ukanda huo. Katika mkutano huo wa 46 wa viongozi wakuu wa jumuiya ya ECOWAS, kila mkuu wa nchi alitumia muda kuwasilisha marejeo juu ya utendaji wa kanda hiyo.
Miongoni mwa mambo makuu yaliyojadiliwa ni pamoja na usalama, utekelezaji unaosuasua kwa sarafu ya pamoja ya kanda na ukosefu wa utulivu wa kisiasa katika kanda hiyo. Viongozi wa kanda hiyo wamekuwa wakishinikiza ushirikiano zaidi katika kanda, uhuru zaidi wa watu, bidhaa na huduma kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Ebola yazidi kuuwa
Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan hata hivyo alisisitiza haja ya mapambano dhidi ya mripuko wa Ebola, unaozidi kuichachafya kanda hiyo. "Kanda yetu inaendelea kukabiliwa na changamoto kubwa zaidi, mojawapo ikiwa ni mripuko wa Ebola. Miezi sita iliyopita imeshuhudia athari mbaya za ugonjwa huo kwa kanda hii. Ugonjwa huo umesababisha vifo zaidi ya 7,000 ukiacha athari mbaya kwa uchumi wetu," alisema rais Jonathan.
Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa katika mkutano huo, katibu mkuu wake wa masuala ya Afrika Magahribi, Mohammed Ibn Chambas, alieleza wasiwasi juu ya masuala makubwa yanayoikabili jumuiya hiyo ya Afrika Magharibi.
"Uasi wa Boko Haram umeendelea kusababisha vurugu na raia wasio na hatia wanaendelea kuuawa. Mwelekeo wa kikanda wa vurugu hizi za itikadi kali unazidi kujidhirisha kila kukicha," alisema mwakilishi huyo wa UN na kuongeza kuwa idadi ya wakimbizi na wanaorejea nchini Chad, Cameroun na Niger inakadiriwa kufikia 142,000 hivi sasa. Nchini Nigeria, wakimbizi wa ndani wankadiriwa kuwa 700,000.
Lakini rais wa Halmashauri kuu ya ECOWAS Kadere Desire Ouadraogo, alieleza matumaini ya kutatuliwa kwa matatizo makuu ya kanda hiyo, yakiwemo ya Guinea Bissau, taifa dogo la Afrika Magharibi lililoshuhudia mkururu wa mapinduzi ya kijeshi. Wanzilishi wa ECOWAS walitizamia kuona jumuiya ya kiuchumi ambako watu wako huru kutoka sehemu moja kwenda nyingine, lakini ndoto hiyo bado haijatimia.
Ufaransa yaitaka Afrika kubeba mziga wake
Wakati huo huo, Ufaransa imeyataka mataifa ya Afrika kuimarisha ushirikiano wa mipakani ili kukabiliana na changamoto za usalama, wakati ikipunguza wajibu wake wa kijeshi katika bara hilo. Waziri wa ulinzi wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian aliwambia viongozi wa Afrika, wachambuzi wa masuala ya usalama na wafanyabiashara waliokutana katika mji mkuu wa Senegal Dakar, kwamba wanapaswa kuanzisha majukwa ya mara kwa mara kubadilishana mawazo na kusaidia kubeba dhamana ya usalama wa Afrika.
Mwandishi:Ben Adam/Iddi Ssessanga/DW Abuja/rtre.
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman