1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiAsia

Viongozi wa dunia wakutana Seoul kuijadili Akili ya Kubuni

21 Mei 2024

Viongozi mbalimbali wa dunia wanatazamiwa kuidhinisha makubaliano mapya ya matumizi ya akili ya kubuni kwenye mkutano wao unaofanyika nchini Korea Kusini kujadili manufaa na hatari zinazoweza kuletwa na teknolojia hiyo

https://p.dw.com/p/4g68t
Akili ya kubuni, akili bandia, akili mnembe
Jinsi mifumo ya akili ya kubuni inavyofanya kazi.Picha: Oliver Berg/dpa/picture alliance

Mkutano huo wa kilele wa Seoul, ambao umeandaliwa kwa ushirikiano wa Korea Kusini na Uingereza, ni muendelezo wa mkutano wa ufunguzi wa Usalama wa Akili ya Kubuni uliofanyika mwezi Novemba mjini Bletchley, Uingereza.

Kwenye mkutano huo wa Bletchley, nchi zilizoshiriki zilikubaliana kushirikiana kudhibiti "janga linalowezekana" kutokea kutokana na teknolojia hiyo kukuwa kwa kasi ya ajabu.

Soma zaidi: Guterres ashitushwa na Israel kutumia akili bandia Gaza

Mkutano wa Seoul ulianza siku ya Jumanne (Mei 21) na ulitatajiwa kuendelea kwa siku mbili. Mkutano huo pia ulifanyika katika wakati ambapo kampuni kubwa za teknolojia ya mawasiliano kama vile Meta, OpenAI na Google zikikaribia kutambulisha matoleo yao mapya ya kile kiitwacho Akili Mnemba.

Yoon, Sunak kuongoza majadiliano

Jioni ya Jumanne, Rais Yoon Suk wa Korea Kusini na Waziri Mkuu wa Uingereza, Rishi Sunak, walitazamiwa kukutana na viongozi wengine wa nchi, wawekezaji wa viwandani na wakuu wa mashirika ya kimataifa kwa mkutano wa njia ya mtandao, ambao nao utafuatiwa na mikutano ya ana kwa ana kati ya mawaziri wa masuala ya dijitali, wataalamu na washiriki wengine hapo kesho.

Wasichana na wanawake wanavyotumia fursa ya teknolojia

"Ni miezi sita tu imepita tangu viongozi wa dunia walipokutana mjini Bletchley, lakini hata ndani ya kipindi hicho kifupi, tayari muonekano wa Akili ya Kubuni umeshabadilika pakubwa. Kasi ya mabadiliko itaendelea kusonga mbele, kwa hivyo kazi yetu nayo inapaswa kusonga mbele pia." Yoon na Sunak walisema kwenye makala yao ya pamoja iliyochapishwa kwenye gazeti la JoongAng ilbo la Korea Kusini na mtandao wa inews wa Uingereza.

Soma zaidi: Umoja wa Ulaya wakubaliana juu ya sheria muhimu ya AI

Ambapo mkutano wa Uingereza ulijikita kwenye masuala ya usalama katika Akili ya Kubuni, ajenda ya mkutano wa wiki hii imetanuliwa kujumuisha pia "ubunifu na ushirikishaji", kwa mujibu wa naibu mkurugenzi wa usalama wa taifa wa Korea Kusini, Wang Yun-jong. 

Wang aliwaambia waandishi wa habari kuwa washiriki wa mkutano huu hawatajadili vitisho vya Akili ya Kubuni pekee, bali pia mambo mazuri yaliyomo ndani yake na vipi teknolojia hiyo inavyoweza kuchangia kwenye ubinadamu katika hali ya uadilifu.

Uhaba wa wafanyakazi roboti zachukua fursa

Ulaya yaidhinisha sheria mpya 

Mawaziri wa masuala ya teknolojia wa Umoja wa Ulaya waliokuwa wanakutana mjini Brussels, Ubelgiji, siku ya Jumanne walitowa idhini yao kwenye kupitishwa Sheria ya Akili ya Kubuni, sheria ambayo ni kubwa kabisa kuwahi kupitishwa kwenye Umoja huo yenye lengo la kuratibu matumizi ya teknolojia hiyo kwenye hali za hatari, kama vile ulinzi na ajira.

Soma zaidi: Waziri Mkuu Sunak kuongoza mikutano ya Akili Bandia

Umoja wa Ulaya unaamini kwamba kwa kuweka sheria kali za Akili ya Kubuni wakati bado ingali mapema, utaweza kukabiliana hatari zinazotokana na teknolojia hiyo kwa wakati na kusaidia kwenye kuunda ajenda ya kimataifa kwenye uratibu wa hiki kiitwacho na wengine kuwa ni Akili Mnemba.

Vyanzo: AP, dpa