Viongozi wa Afrika wataka ufadhili zaidi wa mataifa tajiri
29 Aprili 2024Kwenye Kongamano la Maendeleo ya Kimataifa IDA linaloendelea jijini Nairobi nchini Kenya viongozi hao wamesema ili kufanikisha malengo hayo pana haja ya kufanywa mageuzi kwenye asasi za kimataifa ambazo hufadhili mataifa yanayostawi.
Rais William Ruto wa Kenya aliyefungua rasmi Kongamano hilo la siku mbili, alitangulia kwa kupaza sauti kwa mashirika wafadhili kuitikia mchango wa Chama Cha Maendeleo ya Kimataifa-IDA.
Aidha alielezea kuwa mataifa ya Afrika yanakabiliwa na madeni yanayotishia kusambaratisha chumi zao. Chama cha Maendeleo ya Kimataifa-IDA ni Taasisi ya Benki ya Dunia ambayo hutoa mikopo kwa riba nafuu na za muda mrefu kwa mataifa yanayoendelea.
“Kuwekeza kiwango kikubwa cha fedha kwa IDA ni muhimu. Kikundi cha wataalamu huru wa mataifa ya G20 wanapendekeza kuongezwa mara tatu kwa fedha zinazotolewa kwa IDA kufikia dola bilioni 279 ifikapo mwaka 2030. Tusipuuze ushauri wa wataalam hao,” amesema Rais Ruto.
Matamshi ya Rais Ruto yanajiri huku Mataifa ya Jumuiya ya Afrika yakikabiliwa na mafuriko mabaya kuwahi kushuhudiwa katika historia ya mataifa husika.
Nchini Kenya pekee idadi ya maafa imefikia 100 huku watu waliopoteza makazi wakifikia watu elfu sitini. Hali ambayo wataalam wanasema imechangiwa na mabadiliko ya hali ya hewa.
Iwapo wafadhili wataahidi kutoa kiwango kidogo cha fedha kama viongozi wa Afrika wanavyopendekeza kiwango hicho kitaongezeka maradufu, kwani mwaka 2021 fedha hizo zilifikia dola bilioni 93.
Benki ya Dunia yaahidi kulegeza masharti ya kutoa mikopo
Rais wa Benki ya Dunia Ajay Banga, ameahidi kupunguza mzigo wa masharti yanayotumika wakati wa kutoa mikopo kwa mataifa.
Amesema hatua hiyo itachochea mchakato wa kukopa kwa kasi kwa upande wa mataifa yanayokopa. Fedha hizo hutumiwa na serikali za mataifa yanayoendelea kuimarisha sekta za nishati, afya, kilimo na pia kujenga miundo msingi.
Rais wa Tanzania Samia Suluhu ni mmoja wa viongozi 14 wa Afrika waliohudhuria kongamano hili. Yeye kwa upande wake amesema, “Tunaamini kuwa IDA 21, inastahili kuangazia zaidi mikopo yenye masharti nafuu itakayolipwa kwa miaka 50. Mikopo hiyo itasaidia kwa maendeleo ya mataifa ya Afrika."
Kikundi cha wataalamu huru wa mataifa ya G20 wanapendekeza kuongezwa mara tatu kwa fedha zinazotolewa kwa chama cha IDA kufikia dola bilioni 279 ifikapo mwaka 2030.
Viongozi hawa pia wamependekeza kutumia uanachama wa Umoja wa Afrika kushinikiza mataifa ya G-20 kuipa kipaumbele suala IDA kwenye mikutano yao yote.
IDA ina miradi 75 kote barani Afrika. Chama cha Maendeleo ya Kimataifa –IDA kilianzishwa mwaka 1960 kwa lengo la kupunguza umasikini kwa kutoa mikopo bila riba kwa miradi ya maendeleo inayolenga kuimarisha uchumi, ukuaji, usawa na kuinua hali ya wananchi.