Viongozi kukutana karibuni kuhusu mashariki ya Kongo: Angola
28 Juni 2024Rais wa Angola Joao Lourenco amesema wakati wa ziara yake Cote d'Ivoire kuwa mazungumzo yanaendelea kwa sasa, katika ngazi ya uwaziri, kwa lengo la kuwaleta pamoja wakuu wa nchi za Kongo na Rwanda, kwa mazungumzo ya ana kwa ana kuhusu haja ya kupata amani ya kudumu.
Lakini Waziri Mkuu wa Kongo Judith Suminwa Tuluka amefuta kuwepo mazungumzo yoyote na Rwanda, akitoa wito wa kuchukuliwa hatua kali na vikwazo dhidi ya Kigali.
Angola imekuwa msuluhishi katika mzozo wa eneo la mashariki ya Kongo la Kivu Kaskazini, ambako waasi wa M23 wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda wamekuwa wakipigana na vikosi vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tangu mwishoni mwa mwaka wa 2021.
Juhudi za kidiplomasia zimekuwa zikiendelea kwa miezi kadhaa kuwaleta pamoja Rais Paul Kagame wa Rwanda na Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.