Angola yatarajia mkutano wa Rwanda-DR Congo kupunguza uadui
12 Machi 2024Akizungumza na waandishi wa habari katika mji mkuu wa Angola Luanda, waziri wa mambo ya nje wa Angola Tete Antonio alisema iliamuliwa kwamba rais wa Rwanda Paul Kagame atakubali kukutana na rais wa Congo Felix Tshisekedi siku na tarehe itakayotangazwa na mpatanishi.
Tangazo hilo lilijiri baada ya mkutano uliofanyika Luanda Angola kati ya Rais Paul Kagame na rais wa Angola Joao Lourenco ambaye ndiye mpatanishi aliyeteuliwa na Umoja wa Afrika.
Soma pia: M23 wadhibiti eneo jingine wakati mapigano yakiendelea kwa siku ya tatu Kongo
Wakuu hao wa nchi walikubaliana kuhusu hatua muhimu za kushughulikia mizizi ya machafuko hayo na haja ya kuendeleza michakato ya amani ya mjini Nairobi na Luanda ili kurejesha amani na utulivu katika kanda hiyo.
Ikulu ya rais wa Rwanda ilisema hayo kwenye mtandao wa kijamii wa X, ambao zamani ulijulikana kama Twitter.
Matakwa ya Tshisekedi kabla ya mkutano
Mnamo mwisho wa mwezi Februari, ikulu ya rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ilisema kupitia mtandao wa X, huku ikimnukuu Tete Antonio kwamba "Rais Felix Tshisekedi kimsingi ametoa makubaliano yake ya kukutana na mwenzake wa Rwanda."
Lakini iliongeza kuwa Felix Tshisekedi anahimiza kwanza kabla ya mkutano huo na Rais Kagame, vikosi vya Rwanda RDF viondoke katika ardhi ya Congo na machafuko ya waasi wa M23 yasitishwe.
Kulingana na Umoja wa Mataifa, mapigano kati ya jeshi la Congo na waasi wa M23, ambao wengi wanatoka jamii ya Watutsi, yameongezeka mashariki mwa Congo na kusababisha zaidi ya watu 100,000 kuyakimbia makaazi yao.
Soma pia:
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na mataifa ya Magharibi yanaishutumu Rwanda kwa kuliunga mkono kundi la M23, madai ambayo Kigali inakanusha.
Fahamu pia jinsiVita vya M23 vinaathiri mfumo wa elimu huko Goma, DRC
Mkutano uliojaa matusi kati ya Rais Kagame na Rais Tshisekedi
Rais Kagame na Rais Tshisekedi walikutana mara ya mwisho Februari 16 nchini Ethiopia, pembezoni mwa mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Afrika. Mkutano wao mdogo wa kilele uliandaliwa na Rais Lourenco.
Soma pia: Raia wakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula Goma
Kulingana na vyanzo viwili vya kidiplomasia mjini Addis Ababa, mkutano huo uligubikwa na mvutano mkubwa na ulimalizika kwa "matusi kutoka pande zote mbili".
Baada ya miaka minane ya kimya, waasi wa M23, walianza mashambulizi mwishoni mwa mwaka 2021 na kukamata maeneo makubwa ya Kivu Kaskazini inayopakana na Rwanda.
Mwishoni mwa mwaka 2023, Umoja wa Mataifa ulikadiria kwamba takriban watu milioni saba wameyakimbia makwao nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, waliohama Kivu Kaskazini pekee wakikadiriwa kuwa watu milioni 2.5.
Pata makala zaidi hapa kuhusu mzozo wa Kongo Mashariki
Chanzo: AFPE