1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi hawajui mambo yanayowakabili wasichana, wanawake.

28 Septemba 2017

Viongozi wengi katika mataifa yanayoendelea hawajui maswala yanayowakabili wasichana na wanawake. Hii ni kulingana na ripoti mpya ya utafiti iliyoandaliwa na shirika la utafiti la Ipsos.

https://p.dw.com/p/2kqZ2
Symbolbild Afrika Kinderbräute
Picha: picture alliance/AP Images/S. Alamba

Utafiti huo umeonyesha kuwa, watunga sera katika mataifa yanayoendelea huenda hawana maelezo ya kutosha na ya kuridhisha kuhusu matatizo yanayowakabili wanawake na wasichana ili kusaidia kufikia usawa wa kijinsia.

Ni watunga sera wachache pekee walioweza kukadiria idadi ya wanawake wanaofariki kutokana na matatizo ya uja uzito katika nchi zao, na robo tu walikaribia kukadiria idadi ya ndoa za mapema, kulingana na utafiti iliyofanyiwa  kundi moja linalopigia debe usawa wa kijinsia la Equal Measures 2030.

Utafiti huo ulitilia shaka juu ya jinsi mataifa yanavyoweza kufikia usawa wa kijinsia kufikia mwaka wa 2030, lengo lililojumuishwa katika malengo 17 endelevu ya maendeleo iliyopitishwa na umoja wa mataifa miaka miwili iliyopita, ripoti hiyo imesema.

Ripoti hii ilitolewa wakati wa mkutano mkuu wa wiki hii wa Umoja wa Mataifa jijini Newyork Marekani, ambako malengo hayo yalikubaliwa mwaka wa 2015.

Theluthi mbili ya watunga sera waliohojiwa walisema wanaamini kuna ubora zaidi wa jinsia katika nchi zao sasa kuliko ilivyokuwa miaka mitano iliyopita. Hata hivyo, uchunguzi huo uligawanyika kati ya wanaume na wanawake. Karibu wanane katika ya wanaume kumi wanahisi usawa wa kinjinsia umefikiwa sasa lakini takriban nusu ya wanawake pekee walikubaliana na hilo, ripoti imeonyesha.

Zaidi ya mara mbili ya wanawake kuliko wanaume wanahisi usawa wa kijinsia haujafikiwa au hali imekuwa mbaya zaidi.

Weibliche Genitalverstümmelung Somalia
Msichana akishiriki kwenye majadiliano kuhusu maswala ya wanawakePicha: Getty Images/AFP/N. Sobecki

Mkurugenzi wa kundi linalotetea usawa wa kijinsia la Equal measures 2030 Alison Holder amesema watunga sera wanakuwa vipofu linapokuja swala la usawa wa kijinsia. Theluthi mbili ya watunga sera wanaamini maendeleo yamepatikana lakini hawana ujasiri katika ujuzi wao kutokana na maelezo na takwimu zilizopo. "Tunahitaji picha kamili ikiwa tutaweza kupata nafasi yoyote ya kufikia ahadi zilizowekwa katika malengo endelevu ya maendeleo." Alisema hayo katika taarifa iliyoongozana na ripoti hii.

Utafiti huu uliwahoji watunga sera 109 katika mataifa ya Colombia, India, Indonesia, Kenya na Senegal kuhusu idadi ya wanawake wanaofariki kutokana na matatizo ya uja uzito, viwango vya ndoa za mapema, asilimia ya wanawake wanaofanya kazi na asilimia ya wanawake katika bunge. Wale waliohojiwa ni viongozi wa serikali kuu na za mitaa, wabunge, watumishi wakuu wa umma na watu wenye ushawishi juu ya sera wakiwemo wakuu wa taasisi za biashara, tume au vyama vya wafanyakazi.

Asilimia 6 tu ndani ya asilimia 20 walitoa takwimu sahihi ya kukadiria idadi ya wanawake wanaofariki kutokana na matatizo ya uja uzito na robo tu waliweza kufanya hivyo juu ya swala la ndoa za mapema, ripoti hiyo ilisema. Wachache chini ya thuluthi moja waliweza kufanya makadirio ya karibu ya sehemu ya wanawake wanaofanya kazi.

Kwa mfano makadiro ya watunga sera wa Colombia juu ya ndoa za mapema nchini humo ilianzia kutoka asilimia 4 hadi 80, wakati takwimu halisi ya wasichana walioolewa kabla ya umri wa miaka 18 ni asilimia 23, ripoti hiyo ilisema.

Nchini Kenya, watunga sera walikadiria kuwa sehemu ya viti bungeni vinavyoshikiliwa na wanawake ni kwa kati ya asilimia 6 hadi 90 wakati takwimu sahihi ni asilimia 21, kulingana na ripoti hiyo.

Tofauti kubwa katika majibu hayo inaibua maswali kuhusu iwapo watunga sera wana ufahamu, wanaweza kufikia au wanaongozwa na data husika inayohitajika kutathmini maendeleo ya wasichana na wanawake kuelekea malengo endelevu ya kimaendeleo, ripoti hiyo inasema.

Utafiti huu ulifanywa na watu binafsi na kwa njia ya simu na kampuni ya utafiti ya Ipsos kati ya Julai 21 na Septemba 6.

Mwandishi: Fathiya Omar/RTRE

Mhariri: Iddi Ssesanga