Viongozi Asia ya Kati waitaka Ujerumani kuwatambuwa Taliban
17 Septemba 2024Ujerumani, ambayo kwa miongo miwili mizima ilikuwa na wanajeshi wake waliokuwa sehemu ya uvamizi na ukaliaji ulioongozwa na Marekani nchini Afghanistan imekuwa mkosoaji mkubwa wa utawala wa Taliban.
Kansela Scholz yuko ziarani mjini Astana nchini Kazakhstan katika mkutano na nchi tano za eneo la Asia ya Kati. Afghanistan inapakana na nchi tatu kati ya hizo ambazo ni Turkmenistan, Uzbekistan na Tajikistan.
Hata hivyo, kwenye mkutano huo wa kilele, Scholz alichukuwa tahadhari katika kutoa maoni yake juu ya Afghanistan na badala yake akijielekeza zaidi kwenye ukosoaji wake wa jinsi utawala wa Taliban unavyobana haki za wanawake.
Soma zaidi: Scholz azuru Kazakhstan kuimarisha biashara, ugavi wa mafuta
Kinachotokea nchini Afghanistan hakivumiliki. Ni wazi kwetu kuwa serikali ya Taliban imeingia madarakani kinyume na sheria na kuna mambo mengi yanayotokea huko ambayo yanafadhaisha." Alisema Scholz.
Baada ya miaka 20 ya kuondolewa madarakani kwa nguvu kufuatia uvamizi uliongozwa na Marekani, Taliban iliuchukuwa mji mkuu wa Afghanistan na kurejea tena madarakani pale vikosi vya mataifa ya Magharibi vilipolazimika kuondoka kwa ghafla mwezi Agosti 2021 na kuifanya serikali iliyokuwa ikiungwa mkono na mataifa hayo kuporomoka.
Ziara ya kiuchumi
Ziara ya Kansela Scholz nchini Kazakhstan ilikuwa na dhamira ya kujenga mahusiano ya kiuchumi, hasa kwenye eneo la nishati.
Mjini Astana, alipokelewa na mwenyeji wake, Rais Kassym-Jomart Tokayev, ambapo alisema angelifanya kila awetalo kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na akatowa wito wa ushiirikiano endelevu kwenye masuala ya malighafi.
Soma zaidi: Kansela Olaf Scholz amefanya mazungumzo kuhusu ushirikiano wa kiuchumi na rais wa Kazakhstan
Kazakhstan ni taifa la tatu miongoni mwa mataifa yanayoipatia nishati Ujerumani, baada ya Norway na Marekani. Takribani asilimia 11.7 ya mafuta ya petroli ya Ujerumani yanatokea kwenye taifa hilo la Asia ya Kati, ambalo limechukuwa nafasi ya Urusi tangu uanze uvamizi wa Moscow nchini Ukraine.
Taifa hilo ambalo liliwahi kuwa sehemu ya Shirikisho la Kisovieti lina mpaka wa zaidi ya kilomita 7,600 na Urusi na bado lina mafungamano makubwa na Moscow. Wakati huo huo, imekuwa ikisaka mafungamano ya karibu na mataifa ya Magharibi.
Scholz alituwa nchini Kazakhstan jana akitokea Uzbekistan, na alisaini makubaliano ya kuendelea kupokea mafuta ya Kazakhstan hadi mwishoni mwa mwaka ujao.
Msemaji wa kampuni inayopokea mafuta ya Kazakhstan nchini Ujerumani, Burkhard Woelki, aliliambia shirika la habari la dpa kwamba mkataba huo wa sasa unaipa fursa Kazakhstan kuuza tani 100,000 kwa mwezi hadi mwishoni mwa mwaka 2025.
Kwa mujibu wa vyanzo vya serikali, KazaKhstan iliiuzia Ujerumani tani milioni moja za mafuta ghafi mwaka jana, na mwaka huu imepanga kusafirisha tani milioni 1.4. Mkataba huo pia umeweka uwezekano wa kuongeza kiwango hicho kwa mujibu wa mahitaji.
dpa