Viongozi 11 wa nchi za Balkan waiunga mkono Ukraine
22 Agosti 2023Hati hiyo ya kuunga mkono uadilifu wa Ukraine ilitiwa saini na viongozi kutoka Serbia, Moldova, Montenegro, Romania, Kosovo, Bosnia na Herzegovina, Macedonia ya Kaskazini, Bulgaria na Croatia, pamoja na Ugiriki iliyoandaa hafla hiyo. Rais wa baraza kuu la Umoja wa Ulaya Charles Michel na rais wa halmashuri kuu ya Umoja huo Ursula von der Leyen pia walihudhuria kongamano hilo.
Viongozi hao pia walielezea uungaji mkono na shukran zao kwa juhudi za Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky katika kuweka kanuni za amani kwa mujibu wa mkataba wa Umoja wa Mataifa.
Soma pia: Jeshi la Ukraine lavuka na kuingia katika jimbo la Kherson
Marubani wa Ukraine wa ndege za kivita chapa F-16 kupata mafunzo
Ugiriki ilikuwa imesema kuwa itasaidia kuwapa mafunzo marubani wa Ukraine wa ndege za kivita chapa F-16 na kusaidia katika ujenzi mpya wa Odesa. Siku ya Ijumaa, Ukraine ilipongeza uamuzi wa Marekani wa kuiruhusu Denmark na Uholanzi kupeleka ndege hizo za kivita chapa F-16 nchini Ukraine pindi marubani wake watakapopata mafunzo ya kuzitumia. Waziri wa ulinzi wa Ukraine Oleskii Reznikov amesema ana imani kuwa mataifa zaidi hivi karibuni yatajiunga na kile kinachojulikana kama muungano wa anga kwa kutoa ndege zaidi za kivita chapa F-16 kwa Ukraine.
Soma pia: Ugiriki kuwafunza marubani wa Ukraine kurusha ndege za F-16
Urusi yadai kuzuia uvamizi wa Ukraine
Katika hatua nyingine, gavana wa eneo la Bryansk nchini Urusi Alexander Bogomaz amesema kuwa vikosi vya nchi hiyo vimezuia jaribio la wavamizi wa Ukraine la kuingia katika eneo hilo la Bryansk. Katika ujumbe kupitia mitandao ya kijamii, Bogomaz amesema kuwa wavimizi hao walijaribu kuingia kupitia mpaka wa wilaya ya Klimovsky.
Tazama pia:
Ameongeza kuwa shambulizi hilo lilizuiwa na taasisi mbali mbali za usalama ikiwemo wizara ya Ulinzi, ulinzi wa kitaifa na FSB lakini hatua zinachukuliwa kuhakikisha usalama wa raia. Hata hivyo Ukraine imekanusha kuhusika na mashambulizi hayo na badala yake kuyalaumu makundi ya Urusi yanayompinga rais Vladimir Putin.
Mahakama ya ICC kusikiza pingamizi ya Urusi kuhusu kesi ya mauaji ya kimbari
Mahakama ya Kimataifa ya Haki -ICJ- imesema kuwa itasikiza pingamizi za Urusi kuhusu mamlaka yake katika kesi ya mauaji ya kimbari iliyowasilishwa na Ukraine, katika vikao vitakavyoanza Septemba 18. Ukraine iliwasilisha kesi hiyo muda mfupi baada ya uvamizi wa Urusi kuanza mnamo Februari 24,2022 ambapo iliishtumu Urusi kwa kutumia kwa uongo sheria ya mauaji ya kimbari kuhalalisha shambulizi hilo.