1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikwazo vya silaha Syria kujadiliwa wiki ijayo

16 Machi 2013

Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya watapitia upya mapendekezo ya kuondoa vikwazo vya silaha dhidi ya Syria, baada ya viongozi wa umoja huo kushindwa kukubaliana kuhusu suala hilo jana Ijumaa (15.03.13).

https://p.dw.com/p/17ypL
Baadhi ya viongozi wa Umoja wa Ulaya
Baadhi ya viongozi wa Umoja wa UlayaPicha: Reuters

Ufaransa na Uingereza zimekuwa zinashinikiza pendekezo la kuwapatia silaha waasi wa Syria wanaopambana na utawala wa Rais Bashar al-Assad. Hata hivyo, pendekezo hilo limeungwa mkono na mataifa machache katika mkutano wa siku mbili uliofanyika mjini Brussels, Ubelgiji. Waziri Mkuu wa Uingereza, Dabid Cameron aliuambia mkutano huo kuwa nchi yake inafikiria kuwapatia silaha waasi.

Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya, Herman Van Rompuy amesema viongozi wa umoja huo wamekubaliana kulikabidhi jukumu hilo kwa mawaziri wa mambo ya nje, ambapo watajadiliana katika mkutano wao utakaofanyika Ijumaa na Jumamosi ya wiki ijayo mjini Dublin, Ireland.

Herman Van Rompuy
Herman Van RompuyPicha: Reuters

Hata hivyo, viongozi wengi wa Ulaya wana shaka huenda hatua ya kuondoa vikwazo vya silaha, ikaongeza umwagikaji zaidi wa damu. Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel ameelezea wasiwasi wake kuhusiana na pendekezo hilo. Amesema iwapo Umoja wa Ulaya utakubali kuwapatia silaha waasi wa Syria, washirika wa Rais Assad wanaweza wakafanya hivyo pia. Aidha, Kansela wa Austria, Werner Faymann amesema nchi yake haiko tayari kuondoa vikwazo hivyo.

Mzozo wa Syria waingia mwaka wa tatu

Makubaliano ya pendekezo la kuwapatia silaha waasi wa Syria yameshindwa kufikiwa katika siku ambayo mzozo wa Syria umeingia mwaka wake wa tatu. Wasyria kuzunguka duniani kote walikesha ikiwa ni katika kukumbuka mwaka wa pili tangu kuanza kwa mzozo huo Machi 15 mwaka 2011.

Shirika la kimataifa la Msalaba Mwekundu limewataka viongozi duniani kote kuweka shinikizo kwa utawala wa Syria na upinzani ili kusitisha mashambulizi dhidi ya raia. Ama kwa upande mwingine, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pia limesisitiza umuhimu kwa vyama vyote nchini Lebanon kuacha kujiingiza katika mzozo wa Syria.

Wafanyakazi wa Msalaba Mwekundu na majeruhi wa Syria
Wafanyakazi wa Msalaba Mwekundu na majeruhi wa SyriaPicha: AFP/GettyImages

Wakati huo huo, Syria imesema inaweza ikawashambulia kwa makombora, waasi wanaojificha katika nchi jirani ya Lebanon, kama hawatafukuzwa. Shirika la habari la Lebanon-SANA, limesema waasi hao wamekimbilia Lebanon baada ya mapigano kuzuka kati yao na vikosi vya serikali karibu na mpakani.

Syria yaishuku Jordan, yatangaza kuwashambulia waasi walioko Lebanon

Serikali ya Syria inaishuku nchi jirani ya Jordan kwa kufungua mipaka yake mwezi huu kuruhusu ununuzi wa silaha uliofanywa na Saudi Arabia kutokea Croatia kwa ajili ya kuwapatia waasi.

Rais Bashar al-Assad
Rais Bashar al-AssadPicha: DSK/AFP/GettyImages

Jana Ijumaa(15.03.2013), jeshi la Syria lilianzisha mashambulizi katika maeneo ya mji wa Homs, ikiwemo Baba Amfr, Mji mkongwe na Khaldiyeh. Taarifa hizo ni kwa mujibu wa shirika la Syria la kuangalia haki za binaadamu lenye makao yake London, Uingereza. Kwa mujibu wa shirika hilo, kiasi watu 101 wameuawa jana katika sehemu mbali mbali za nchi hiyo.

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa watu elfu 70 wameuawa kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria na wengine zaidi ya milioni 1.1 wamekimbilia kwenye nchi jirani. Umoja huo umesema pia kuwa watu milioni nne wanahitaji msaada wa haraka wa kibinaadamu.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,DPAE
Mhariri: Sekione Kitojo