1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya wasaka msimamo wa pamoja

15 Machi 2013

Tofauti za maoni kati ya viongozi wa Umoja wa ulaya hazijajitokeza pekee katika masuala ya kiuchumi-hata katika suala la Syria maoni yanatofautiana

https://p.dw.com/p/17yQN
Kansela Angela Merkel,spika wa bunge Martin Schulz na rais Francois Hollande wa UfaransaPicha: Reuters

Kwa mara ya kwanza viongozi wa mataifa 27 ya Umoja wa Ulaya wanakutana bila ya shinikizo la mgogoro wa fedha,hali inayoupatia mkutano huo wa kilele sura ya mkutano wa kisiasa hata kama hakuna uamuzi thabiti utakaopitishwa.

Kipa umbele ni namna ya kuleta uwiano kati ya juhudi za kuimarisha bajeti na ukuaji wa kiuchumi-hali inayowatenganisha kwa upande mmoja wale wanaofuata kambi ya wanaopigania hatua za kufunga mkaja,wanaoongozwa na kansela Angela Merkel na kwa upande wa pili kambi ya wale wanaodai kufuata mkondo wa mambo ulivyo wakiongozwa na rais wa Ufaransa,Francois Hollande.

Masuala ya ukosefu wa ajira, dhiki na kuzorota uchumi ni miongoni mwa mada zilizohodhi mikutano ya viongozi wa Umoja wa Ulaya.Yadhihirika kana kwamba hakuna kati ya viongozi wa Umoja huo anaethubutu kulitaja neno "kuzatiti".

Hata mjini Brussels maelfu waliandamana jana dhidi ya hatua za kupunguza matumizi katika wakati ambapo viongozi walikuwa wakijadiliana. Hata kansela Angela Merkel ambae hadi wakati huu alikuwa akitajwa kuwa kiongozi anaependelea hatua za kufunga mkaja-hakusema kitu,ameungama japo si moja kwa moja misimamo ya nchi za Ulaya inatofautiana. Kansela Angela Merkel amesema:"Tunaweza tu kuyafikia malengo tuliyojiwekea,ambayo ni pamoja na ukuaji wa kiuchumi na hasa kubuni nafasi nyingi zaidi za kazi na bajeti madhubuti,ikiwa tutakuwa na mtazamo wa aina moja wa sera za kiuchumi."

Umoja wa ulaya unakabiliana pia na upinzani wa bunge

Van Rompuy PK beim EU Gipfel in Brüssel
Rais wa Umoja wa Ulaya Herman Van RompuyPicha: Reuters

Mbali na upinzani wa majiani,viongozi wa Umoja wa Ulaya wanakabiliwa pia na upinzani wa bunge la Ulaya kuhusu bajeti ya mwaka 2014 hadi 2020 iliyopitishwa mwezi uliopita. Bajeti hiyo ni haba ikilinganishwa na pendekezo la halmashauri kuu ya Umoja wa ulaya na kuna pengo pia kati ya uwezo wa malipo na majukumu yaliyoko. Bunge la Ulaya kwa hivyo limekataa kuidhinisha mswaada huo wa bajeti.

Siasa ya nje pia inatarajiwa kugubika mkutano huo wa viongozi wa Umoja wa Ulaya: Rais wa Ufaransa Francois Hollande amewaomba viongozi wenzake waondowe marufuku ya silaha kwa upande wa upinzani nchini Syria. Pindi akishindwa kuwatanabahisha wenzake,anasema Francois Hollande,basi Ufaransa itakuwa tayari kuwajibika na kuwapatia silaha wapinzani wa Syria.

Mwandishi: Christoph Hasselbach/Hamidou Oummilkheir

Mhariri: Mohammed Khelef