1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya usalama Misri hukamata na kutesa watoto

23 Machi 2020

Shirika la Human Rights Watch limewakosoa majaji na waendesha mashtaka nchini Misri kwa kufumbia macho vitendo vya ukamataji kiholela, kuwapoteza na kuwatesa watoto wenye umri wa hadi miaka 12 na vikosi vya usalama.

https://p.dw.com/p/3ZuV9
Deutschland Compact with Africa Initiative in Berlin | Agyptischer Präsident al-Sissi
Picha: picture-alliance/AFP/J. Macdougall

Kufuatia madai hayo, ripoti hiyo iliyochapishwa Jumatatu (23.03.2020) imetoa mwito kwa Marekani, Ufaransa na mataifa mengine ya Umoja wa Ulaya kusitisha misaada kwa vikosi hivyo vya Misri hadi pale mamlaka zitakapochukua hatua madhubuti za kumaliza unyanyasaji dhidi ya watoto pamoja na kuwawajibisha wahusika wa unyanyasaji huo.

"Watoto wanatajwa kukabiliwa na mateso mbalimbali ikiwa ni pamoja na kumwagiwa maji usoni huku wakiwa wamefungwa kitambaa na kuteswa kwa umeme kwenye ulimi na sehemu ya siri, lakini vikosi vya usalama vya Misri haviwajibishwi” amesema Bill Van Esveld, mkurugenzi wa masuala ya haki za watoto katika shirika hilo la Human Rights Watch.

Msemaji kutoka wizara ya mambo ya ndani ya Misri inayosimamia jeshi la polisi hakupatikana mara moja kuzungumzia madai hayo. Kwenye ripoti hiyo yenye kurasa 43, kundi hilo la haki za binaadamu lenye makao yake mjini New York limesema limerekodi visa 20 vya mateso dhidi ya watoto wa kati ya miaka 12 na 17 ambavyo hufanyiwa baada ya kukamatwa. Watoto 15 miongoni mwao walisema waliteswa wakati walipokuwa kwenye mahabusi walizozuiwa kabla ya kusomewa mashitaka, na hususan wakati wanapohojiwa, limesema shirika hilo.

Ägypten - Explosion tötet Polizisten in Kairo
Vikosi vya usalama vya Misri vinalaumiwa kwa kuwakamata, kuwatesa na kuwapoteza watoto huku majaji na waendesha mashtaka wakifumbia macho.Picha: picture-alliance/Xinhua

Watoto saba walisema maafisa wa usalama waliwatesa kwa vifaa vya umeme. Kundi hilo lilimnukuu mvulana mmoja wa miaka 16 wakati akiwaambia wazazi wake kwamba ana wasiwasi kwamba "huenda hataweza kuoa ama kupata watoto" kutokana na kile ambacho vikosi hivyo vya usalama walimfanyia wakati alipokuwa mahabusu.

Wanaharakati pia hufungwa kiholela

Shirika hilo limesema kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali linalotoa msaada kwa watoto wanaoishi mitaani la Belady walikusanya taarifa kutoka kwa watoto, familia zao na mawakili wa utetezi wakitumia nyaraka za mahakama, rufaa kwa mamlaka, rekodi ya tiba na video. Aya Hijazi, mkurugenzi mwenza wa shirika hilo la Belady amesema "matukio ya kutisha ya watoto hao pamoja na familia zao yanafichua namna ukandamizaji wa vikosi vya usalama vya Misri ulivyowafanya watoto kupitia mateso makubwa.

Ägypten Kairo Richter bei Urteil gegen Mohamed Mursi
Majaji na waendesha mashtaka nchini Misri wanadaiwa kufumbia macho vitendo vya ukamataji kiholela, upotezaji na utesaji watoto na vikosi vya usalama chini ya utawala wa rais Abdel-Fattah al-Sisi.Picha: picture-alliance/ZUMA Press

Hijazi ambaye ni raia wa nchi mbili, Marekani na Misri na aliwahi kuzuiwa kizuizini kwa karibu miaka mitatu kufuatia madai yanayohusiana na shirika hilo la Belady ambalo kwa Kiarabu jina hilo likimaanisha "Taifa letu". Alikamatwa pamoja na mumewe na watu wengine sita Mei 2014 kwa madai ya kuwanyanyasa watoto. Alishitakiwa na kuachiwa miaka mitatu baadaye.

Kulingana na ripoti hiyo ya Human Rights Watch, kijana wa miaka 17, Belal B wakati alikamatwa na vikosi vya usalama na kumuweka kwenye chumba cha mahabusu ambacho mfungwa hutengwa na wenzake kilichopo kwenye kituo cha polisi cha Cairo. Alisema hakujua chochote kuhusu wazazi wake na wala wazazi wake hawakujua chochote kumhusu yeye. Alinukuliwa na shirika hilo akisema "maafisa hao walinifunga kwa kamba kwenye kiti kwa siku tatu na kumsababishia maumivu makubwa sana".

Kundi hilo lilisema mfumo wa makosa ya uhalifu nchini Misri umeshindwa kuchunguza madai hayo dhidi ya watoto. Ripoti hiyo imedai kwamba mwendesha mashitaka katika kesi moja alimtishia kijana mmoja kwamba atamrejesha kwa "afisa wa polisi" aliyemtesa iwapo atakataa kukiri madai dhidi yake.

Chanzo: HRW