Wanaharakati vijana wataka makubaliano ya amani Gaza
6 Agosti 2024Miongoni mwa wanaharakati hao, ni raia hawa wa Israel wenye asili ya Palestina ambao ni na Amira Mohammed na wamekuwa wakiandaa vipindi hivyo vya sauti vinavyofahamika kama "podcast" kwa lengo la kukabiliana na hali ya mgawanyiko wa kisiasa inayoshuhudiwa nchini humo.
Wazazi wa mjasiriamali na mwanaharakati mwingine anayetetea amani Maoz Inon walikuwa miongoni mwa wahanga wa kwanza wa mashambulizi ya Hamas nchini Israel asubuhi ya Oktoba 7 mwaka jana. Siku mbili baada ya mkasa huo, licha ya maumivu makubwa aliyokuwa nayo, ilikuwa wazi kwamba hakutaka kulipiza kisasi.
Inon alisema kisasi hakingeliweza kuwarudisha wazazi wake wala kuwarudisha Waisraeli na Wapalestina wengine ambao wamepoteza maisha yao.
Akisimulia kwenye vipindi hivyo, Inon alielezea kuwa usiku wa mauaji hayo, alipata njozi na aliona ardhi iliyojaa damu nyingi. Anasema yeye na watu wote ulimwenguni waliojeruhiwa na vita walikuwa wakilia.
Soma pia:Shambulizi la Israel la leo lauwa watu 18 Gaza
Machozi yao yalishuka usoni hadi kwenye miili yao, yaliwaosha na kuwaponya, kisha machozi hayo yalishuka na kusafisha damu yote ilikuwa imetapakaa chini. Inon amesema haikuwa ndoto mbaya, bali maono ya mustakabali mwema bila ya vitendo vya umwagaji damu.
Katika kipindi hicho, mwandishi wa Palestina Hamze Awawde amesema kilichomsukuma kuwa mwanaharakati wa amani ni kwa sababu anaamini kuwa matumaini sio tu hisia bali ni hatua unazozichukua, huku akisisitiza kuwa kusubiri suluhisho la mataifa mawili bila hatua zozote, ni sawa na kusubiri treni bandarini.
Utambulisho wa kisiasa
Awade na Inon wana matumaini ya kuona vita vya Gaza ambavyo vimegharimu maisha ya karibu watu 40,000 vinasitishwa. Na ndio maana walialikwa kwenye vipindi hivyo vilivyoanzishwa mwezi Oktoba mwaka 2023, mara baada ya shambulio lililoongozwa na Hamas huko kusini mwa Israel. Ujerumani, Marekani, Umoja wa UIaya na mataifa mengine ya magharibi yameirodhesha Hamas kama kundi la kigaidi.
Waanzilishi wawili wa vipindi hivyo, Amira Mohammed na Ibrahim Abu Ahmad, ni miongoni mwa Waarabu wengi wenye uraia wa Israel na wanaoishi nchini humo.
Kulingana na Ofisi Kuu ya Takwimu ya Israel, watu hao wanajumuisha karibu asilimia 17 ya idadi ya watu. Kwa jumla, angalau asilimia 21 ya watu wanaoishi Israel ni Waarabu.
Amira na Ibrahim wanajitambulisha kama Waisraeli wenye asili ya Kipalestina. Tafiti zinaonyesha kwamba watu wengi kwenye jamii hiyo hujinasibu hivyo.
Lakini kisiasa, ni utambulisho wanaopaswa kuupigania, kwani taifa la Israel halitambui utambulisho wa raia wake kuwa na asili ya Palestina. Badala yake, inawataja kama "Waisraeli Waarabu."
Soma pia:Kiiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh azikwa baada ya kuuawa nchini Iran
Katika mahojiano na DW, Amira anaeleza kwamba ana imani Waisraeli wenye asili ya Palestina wanaweza na wanapaswa kuchukua jukumu muhimu katika mzozo wa Mashariki ya Kati hasa kutokana na utambulisho wao.
Amira na Ibrahim wanalenga kuwepo mustakabali mwema badala ya mgawanyiko uliopo sasa. Wanakosoa mtazamo wa Magharibi wa kuunda makundi mawili mithili ya mechi ya kandanda: Wale wanaounga mkono Israel au Palestina. Wanaharakati wameyataka mataifa ya Magharibi kutumia majukwaa yao kukosoa pande zote kwa usawa na bila upendeleo.
Mbinu yao imeonekana kuwa yenye mafanikio. Kwani vipindi vyao vimejizolea umaarufu mkubwa na sasa vikiwa na wasikilizaji 180,000 kwa kila kipindi na karibu wafuasi 30,000 kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram.
Hata hivyo, licha ya mafanikio hayo, wanaharakati hao wawili hukabiliana kila siku na vikwazo. Kumekuwa na upinzani kutoka pande zote, Mohammed anasema anapozungumza Kiarabu hadharani, Waisraeli humtazama kwa hofu. Na anapozungumza Kiebrania bila lafudhi ya Kiarabu, Wapalestina nao hawamwamini.