Kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh auwawa Iran
31 Julai 2024Hadi sasa hakuna aliyekiri mauaji hayo, vidole vyote vinaelekezwa kwa Israel ambayo imebandika kwenye ukurasa wake wa Facebook picha ya Haniyeh ikiwa na maneno "ameangamizwa".
Mengi zaidi yatakuja kufahamika baadaye kuhusu mashambulizi yaliyomuua mmojawapo wa viongozi wakubwa wa mapambano dhidi ya ukaliaji wa Israel kwenye ardhi ya Palestina, ambaye mataifa kadhaa ya Magharibi yanamtambua kama kiongozi wa kundi la kigaidi, lakini kwa sasa kinachojulikana ni kwamba Jeshi la Mapinduzi la Iran limethibitisha kifo cha Haniyeh, aliyekuwa na umri wa miaka 62.
Israel yasema imemuua kamanda wa Hezbollah ndani ya Lebanon
Taarifa zinatafautiana juu ya hasa nini kilichopelekea mauaji hayo: ikiwa ni kombora kutoka nje, ndege isiyo na rubani, au mauaji ya moja kwa moja, kama ambayo yamewahi kuwatokezea watu ambao Israel inawatambuwa kuwa maadui zake ndani ya ardhi ya Iran.
Haniyeh aliyechukuliwa kama taswira ya diplomasia ya kimataifa ya Hamas, aliuawa mnamo saa nane usiku, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Iran. Vyombo hivyo vinasema wakati wa mauaji hayo yaliyomuondowa pia mmoja wa walinzi wake, Haniyeh alikuwa akikaa kwenye makaazi maalum ya maveterani wa vita kaskazini mwa mji mkuu, Tehran.
Iran imesema inachunguza mauaji ya Haniyeh
Jeshi la Mapinduzi la Iran limesema uchunguzi zaidi unaendelea na matokeo yake yatatangazwa baadaye, ingawa tayari inafahamika kuwa mazishi ya Haniyeh na mlinzi wake huyo yatafanyika mjini Tehran.
Kwa mujibu wa chombo cha habari cha NourNews, ambacho kina mafungamano na Baraza Kuu la Usalama la Iran, makaazi ya Haniyeh yalishambuliwa kwa chombo kutoka angani, huku kikiongeza kwamba "mashambulizi hayo yalikuwa kamari ya hatari dhidi ya uwezo wa Tehran kushambulia."
Operesheni ya Israel yaua Wapalestina 300 Khan Younis
Kwa upande wake, jeshi la Israel limejizuwia hadi sasa kutoa tamko lolote zaidi ya kusema kuwa linafanya tathmini ya kina. Hata hivyo, ukurasa wa Facebook wa serikali ya Israel umebandika picha ya Haniyeh ikiwa na maneno "ameangamizwa" juu yake.
Kundi la Hamas laapa kuendelea na operesheni yake katika vita vya Gaza
Ama kwa upande wa kundi la Hamas, umesema kwamba utaendelea na operesheni yake kama kawaida kwenye vita vya Gaza, ukisisitiza kwamba una uhakika wa ushindi.
Taarifa za mauaji ya Haniyeh, ambazo zilitoka chini ya masaa 234 tangu Israel kudai kwa imemuua kamanda wa ngazi za juu wa kundi la Hizbullah nchini Lebanon waliyesema alihusika na mashambulizi kwenye Milima ya Golan, huenda zikawa na athari ya moja kwa moja kwenye upatikanaji wa makubaliano ya kusitisha vita vya Gaza.
Israel yaapa kulipiza kisasi baada ya vijana 12 kuuawa
Wakati huo huo, mashambulizi kwenye ardhi ya Iran na mauaji ya mmoja wa washirika wake wa karibu yanaiweka Tehran kwenye nafasi ya kuchukuwa hatua za kulipiza kisasi dhidi ya Israel, ambayo ilikuwa ikimuwinda Haniyeh tangu mashambulizi ya Oktoba 7.
Vyanzo: AP/AFP