1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUfaransa

Uwanja wa ndege wa New Caledonia kuendelea kufungwa

Saleh Mwanamilongo
24 Mei 2024

Uwanja wa ndege wa kimataifa katika mji mkuu wa New Caledonia, Noumea, utasalia kufungwa kwa safari za ndege za kibiashara hadi Jumanne wiki ijayo.

https://p.dw.com/p/4gG0j
Ufaransa yapeleka wanajeshi zaidi ya elfu tatu kurejesha utulivu New Caledonia
Ufaransa yapeleka wanajeshi zaidi ya elfu tatu kurejesha utulivu New CaledoniaPicha: Manon Cruz/REUTERS

Hatua hiyo inaongeza muda wa kufungwa kwa karibu wiki mbili kwa uwanja wa ndege wa Noumea, baada ya safari za ndege kusimamishwa Mei 15 kutokana na ghasia mbaya zilizozuka katika eneo hilo la Pasifiki linalomilikiwa na Ufaransa.

Charles Roger, mkurugenzi wa bodi inayo simamia uwanja huo wa ndege ameliambia shirika la habari la AFP kwamba safari zote za ndege za kibiashara zimesimamishwa hadi Jumanne ya wiki ijayo.

Ufaransa imetuma wanajeshi wapatao 3,000 katika eneo hilo kwa nia ya kurejesha hali ya utulivu baada ya ghasia za zaidi ya wiki moja ambazo zimesababisha vifo vya takriban watu saba.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ambaye amemaliza ziara yake huko New Caledonia amesema hatua zaidi zitachukuliwa ilikurejesha utulivu.

"Ninachoomba, mara moja, ni vizuizi vya barabarani viondolewe. Na kila kiongozi wa kisiasa anayehusika lazima atoe wito huu wa wazi kuhusu utulivu. Hatua inayofuata ni kwamba tutainua hali ya hatari kwa ngazi ya tatu. Baadaye tunahitaji kufufua mazungumzo kwa ajili ya makubaliano ya kina, ikiwa ni pamoja na wanaotaka kujitenga. Pia nimekubali kuundwa kwa kamati ya usuluhishi.", alisema Macron. 

Mwendesha mashataka wa New Caledonia amesema leo Ijumaa kwamba mtu mmoja ameuliwa kwa kupigwa risasi na polisi mjini Noumea.

Nchi za Pasifiki zaondoa raia wake Noumea

Ghasia zimeikumba New Caledonia kwa zaidi ya wiki kufuatia sheria tata ya uchaguzi
Ghasia zimeikumba New Caledonia kwa zaidi ya wiki kufuatia sheria tata ya uchaguziPicha: Delphine Mayeur/AFP

Tangu Jumanne, New Zealand na Australia zimekuwa zikifanya safari maalum za kuwarejesha nyumbani mamia ya watalii ambao ni raia wake waliokwama kutokana na machafuko hayo. Machafuko hayo yaliokitikisa New Caledonia yalichochewa na upinzani dhidi ya mageuzi yenye utata ya sheria ya uchaguzi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia Penny Wong amesema safari za ndege za kuwaondoa raia wa nchi yake zilipangwa kuendelea leo Ijumaa.

Tangu Mei 13, mamia wamejeruhiwa huku kukiwa na uporaji na mapigano yaliyochochewa na mpango wa mageuzi ya sheria ya upigaji kura wa Ufaransa. New Caledonia imetawaliwa na Ufaransa tangu miaka ya 1800, lakini Wenyeji wa jamii ya Kanak wengi bado wanachukia mamlaka ya Ufaransa juu ya visiwa vyao na wanataka kujiongoza wenyewe au uhuru kamili.

Ufaransa ilikuwa imepanga kutoa haki za kupiga kura kwa maelfu ya wakaazi wa muda mrefu wasio wazawa, jambo ambalo jamii ya Kanak imesema lingepunguza ushawishi wa kura zao.