Utawala wa kijeshi Guinea wamteua Oury Bah kuwa Waziri Mkuu
28 Februari 2024Katika hotuba ya televisheni, msemaji wa utawala huo wa kijeshi unaoongozwa na Kanali Mamady Doumbouya amesema Amadou Oury Bah, mchumi na aliyekuwa wakati mmoja kiongozi wa upinzani, ameteuliwa kuhudumu kama waziri mkuu na mkuu wa serikali.
Doumbouya ameongeza kuwa waziri mkuu huyo mpya atapewa jukumu la kushughulikia mvutano na vyama 13 vya wafanyikazi vilivyoitisha mgomo wa kitaifa ulioanza siku ya Jumatatu.
Soma pia: Idadi ya waliokufa kutokana na moto Guinea yafikia 23
Vyama vya wafanyikazi vinashinikiza kuachiliwa huru kwa katibu mkuu wa muungano wa wanahabari wa Guinea Sekou Jamal Pendessa, kushuka kwa bei ya vyakula, kuondolewa kwa udhibiti wa vyombo vya habari na mtandao wa intaneti pamoja na kutimizwa ahadi ya nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa umma.
Shule, maduka, masoko na barabara katika mji mkuu Conakry zimesalia tupu huku hospitali zikitoa huduma ndogo ndogo pekee.