Ushindi wa Joe Biden: Huruma imeshinda urais
8 Novemba 2020Wakati Joe Biden anapowahutubia Wamarekani wakati wa janga la virusi vya corona, mara nyingi anachukuwa muda kuelezea huruma yake. Nchini Marekani, zaidi ya watu 230,000 wamefariki kutokana na ugonjwa wa virusi hivyo.
Mwishoni mwa mwezi Oktoba, Biden alizungumzia mzozo wa virusi vya corona katika mji wake wa nyumbani wa Wilmington, Delaware na kutoa salaam za pole kwa kila mtu ambaye alipoteza mpendwa wake kutoka na ugonjwa wa covid-19.
Soma pia: Viongozi wa dunia wampongeza Biden, wataka umoja
Wakati akifanya kampeni kuwa rais ajaye wa Marekani, alilenga kutuma ujumbe kinzani kwa ule unaotolewa na rais Donald Trump, aliewambia Wamarekani kutoruhusu janga la Covid-19 kuwadhibiti, na kwamba hakukuwa na haja ya kuuogopa ugonjwa huo.
Joe Biden kwa upande mwingine, amewahimiza watu kuvaa barakoa, kuchukulia kwa uzito suala la kuweka umbali kati ya mtu na mtu, na haoni aibu kujumuika na watu asiowajua katika huzuni. Anajua huzuni ya kumpoteza mwenza, kumzika mtoto, Biden alikaribia kuachana na siasa mara mbili kwa sababu ya hayo.
Mara ya kwanza ilikuwa katika msimu wa baridi mwaka 1972. Alikuwa na umri wa miaka 29 tu alipoamua kugombea dhidi ya seneta mrepublican wa muda mrefu wa jimbo Delaware. Akiwa na wanafamilia wengi katik nafasi za wapiga kampeni na licha ya kuwa na pesa kidogo, Biden alishinda uchaguzi wa Novemba.
Soma pia:Maoni: Rais mpya - lakini hakuna mshindi
Wiki chache tu baadae, alikumbwa na janga lililombadilisha milele. Mke wake Neilia na mtoto wao wa kike wa mwaka mmoja Naomi, walifariki katika ajali ya gari, ambayo pia iliwaacha watoto wao wa kiume Beau na Hunter wakiwa na majeraha mabaya.
Ingawa Biden alitaka kujiuzulu, alishawishiwa kuingia ofisini na aliapishwa akiwa hospitali ambako watoto wake wa kiume walikuwa wakitibiwa. Seneta huyo kijana alisafiri kati ya Wilmingotn na Washington DC.
Dada yake Valerie alihamia nyumbani kwake kumsaidia na watoto na alikaa hadi 1977, wakati Biden alipomuoa Jill Jacobs, ambaye alizaa naye mtoto wa kike, Ashley.
Mara ya pili ilikuwa miongo kadhaa baadae. Mwaka 2015, Biden alikuwa makamu wa rais akifanya kazi na rais wa wakati huo Barack Obama kupitisha sheria ya bima ya afya ya gharama nafuu, ambayo iliwezesha huduma za afya kuwafikia mamilioni ya watu kutoka familia zenye kipato cha chini.
Soma pia: Joe Biden ni rais mteule wa Marekani
Upendo usio na ulaghai, huduma bila kujijali
Wakati Biden akijaribu kuhakikisha wengine wanapata huduma walizozihitaji, mtoto wake mkubwa zaidi wa kiume Beau alikufa kutokana na saratani ya ubongo. Joe Biden aliekuwa amepanga kugombea urais katika uchaguzi wa 2016, aliamua kwamba alihitaji muda zaidi kuwa nyumbani na familia yake.
Siku chache kabla ya kumalizika kwa muda wake kama makamu wa rais, Obama alimtunukuu Biden Medali ya rais ya Uhuru. "Kumjua Biden ni kujua upendo usio na ulaghai, huduma bila kujijali, na kuishi maisha kikamilifu," alisema Obama.
Ukweli kwamba Wademocrat walimchagua Biden kama mgombea wao wa urais - badala ya mmoja ya wagombea vijana au wasio weupe walioshiriki jukwaa la mijadala na Biden, haukuwa wa kushangaza, kwa mujibu wa Mitechell McKinney, profesa wa chuo kikuu cha Missouri ambaye utafiti wake unajikita kwenye midahalo ya urais na matamshi ya wagombea.
Soma pia: Joe Biden bado anahitaji uvumilivu
McKinney anamchukulia Biden kama mwanasiasa mwerevu, mwenye huruma ambaye ni tofauti kabisaa na Trump, aliependa kumuita mpinzani wake kama "Joe anaejikongoja." Ushindi wa Biden ni ishara ya wazi ya kile taifa linachokitamani kwa sasa ktika muktadha wa uongozi, anasema McKenney.
Biden anajulikana kwa kufanya kazi vizuri na watu ambao huenda wasikubaliane naye, anasema mchambuzi wa masuala ya kisiasa Bruce Buchanan, katika mazungumzo na DW. Kabla ya uchaguzi, baadhi ya maseneta wa Republican waliashiria watakuwa tayari kushirikiana na Biden, iwapo atakuwa rais.