1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi,China zazuia juhudi za vikwazo kwa Mali

Angela Mdungu
12 Januari 2022

Urusi na China jana Jumanne zilizuia juhudi za baraza la usalama la UN kuunga mkono vikwazo vipya dhidi ya Mali baada ya viongozi wa kijeshi wa nchi hiyo kuahirisha uchaguzi uliokuwa ufanyike mwezi ujao hadi mwaka 2026

https://p.dw.com/p/45PqY
Ghana Accra | Economic Community of West African States | ECOWAS
Picha: IVORY COAST PRESIDENTIAL PRESS SERVICE/REUTERS

Uamuzi huo wa kusogeza mbele uchaguzi unatajwa kuwa ni pigo kwa harakati za kurejesha demokrasia kwenye taifa hilo la Afrika ya Magharibi lenye mzozo.

Mara baada ya majadiliano ya siri kuhusu pendekezo la Ufaransa lililoidhinisha vikwazo vilivyowekwa na Jumuiya ya kiuchumi ya Mataifa ya Magharibi ECOWAS, balozi wa Kenya katika umoja wa Mataifa Martin Kimani alisema amefadhaishwa kuwa baraza la usalama la umoja wa mataifa limeshindwa kukubaliana na kile alichokiita taarifa ya kiungwana iliyotolewa kwa vyombo vya habari

Kimani amesema, kushindwa baraza la Umoja wa Mataifa kuiunga mkono Jumuiya ya ECOWAS kumeyachochea mataifa matatu ambayo ni wanachama wake Kenya, Ghana na Gabon kuzungumza na waandishi wa habari kuunga mkono kikamilifu msimamo ya jumuiya hiyo ya kieneo. Hii ni pamoja na kuziwekea vikwazo mamlaka za kijeshi za Mali ili kuhakikisha mabadiliko ya haraka kuelekea kwenye utawala wa kikatiba

Mali imekuwa ikipambana kuyadhibiti makundi ya waasi yenye itikadi kali tangu mwaka 2012. Waasi wenye msimamo mkali waliondolewa mamlakani katika miji ya kaskazini katika operesheni maalumu iliyoongozwa na Ufaransa, lakini baadaye walijipanga jangwani na kuanzisha mashambulizi kwa jeshi la Mali na washirika wake.

Awali utawala wa kijeshi  ulikubali kufanyike uchaguzi mpya mwishoni mwa mwezi Februari lakini kwa sasa uongozi unasema, uchaguzi wa rais hautofanyika  hadi mwaka 2026 kutokana na ukosefu wa usalama unaozidi kushamiri nchini humo.

Jeshi kuendelea kuongoza kwa miaka mitano ni kuwashikilia mateka raia 

Jumapili, viongozi wa jumuiya ya kiuchumi ya Afrika magharibi walijibu wakiita hatua hiyo ya kucheleweshwa kwa uchaguzi kuwa ni hatua isiyokubalika na kwamba kufanya hivyo kunamaanisha kuwa serikali ya kijeshi isiyo na uhalali ya Mali itaendelea kuwashikilia mateka waia wa Mali kwa miaka mitano ijayo na kisha wakatangaza vikwazo vipya vikiwemo vya kibiashara na misaada kwa Mali. Pia Jumuiya hiyo ilitangaza kufunga mipaka ya ardhi na nchi kavu katika nchi nyingine zinazopakana na Mali.

Putschistenführer Assimi Goita in Mali als Staatschef vereidigt
Rais wa mpito wa Mali Assimi GoitaPicha: Habib Kouyate/XinHua/dpa/picture alliance

Hatua hiyo ya ECOWAS iliungwa mkono na Marekani, Ufaransa, Uingereza na mataifa mengine wanachama wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa huku yakikosoa vikali uwepo wa kampuni binafsi ya kijeshi ya ulinzi ya Wagner ya Urusi nchini Mali. 

Naye waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi, Sergey Lavrov amesema kuwa kampuni hiyo ina uhalali wa kisheria kuwepo Mali kwani ilialikwa na serikali  na amesisitiza kuwa serikali ya Urusi haihusiki