ECOWAS yaanza kutekeleza vikwazo vyake dhidi ya Mali
11 Januari 2022Akihubutia taifa kupitia televisheni usiku wa kuamkia leo, kiongozi wa kijeshi nchini Mali, Kanali Assimi Goita amesema vikwazo vya Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi - ECOWAS dhidi ya nchi yake sio halali na kwamba Mali ipo tayari kwa mazungumzo.
''Ninawaambia, ijapokuwa tumehuzunishwa na baadhi ya hatua zisizo za kiutu na zisizo halali za jumuiya hiyo, lakini Mali ipo tayari kwa mazungumzo na jumuiya ya ECOWAS, ili kufikia muafaka wa maslahi ya watu wa Mali na kuheshimu kanuni za kimsingi za jumuiya yetu.'',alisema Goita.
Soma pia: ECOWAS yafunga mipaka yake na Mali
Ufaransa na Marekani zaiungamkono Ecowas
Assimi Goita, kiongozi wa sasa wa Mali na mmoja wa makanali waliomwondoa madarakani Rais Ibrahim Boubacar Keita mnamo Agosti 2020, ametoa wito wa utulivu akiongeza kuwa Mali ina mbinu za kuhimili vikwazo ilivyowekewa hivi karibuni.
Shirika la ndege la Cote d'Ivoire lilisitisha safari zake za mji mkuu wa Mali Bamako. Safari kutoka Senegal pia zilivurugika. Shirika la ndege la Ufaransa pia limefuta safari zake, kwa sababu ya vitisho vya kiusalama.
Marekani imesema inaunga mkono vikwazo vikali vilivyotangazwa na Jumuiya ya ECOWAS dhidi ya Mali katika kujibu jaribio la utawala wa kijeshi nchini humo kurefusha uwepo wake madarakani.
Hayo yameelezwa na msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni wa Marekani Ned Price ambaye pia amezungumzia kuunga mkono wasiwasi wa Jumuiya ECOWAS juu ya taathira za kukaribishwa nchini Mali kwa kampuni ya ulinzi binafsi kutoka Urusi ya Wagner.
Soma pia: Mpango wa kuchelewesha uchaguzi wapingwa Mali
Guinea yakaidi kufunga mipaka yake na Mali
Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi - ECOWAS ilitangaza vikwazo vikali dhidi ya Mali ikiwemo kusitishwa miamala ya kifedha, na kufunga mipaka yake ya ardhini na angani kutokana na mamlaka za mpito za nchi hiyo kushindwa kuandaa uchaguzi wa kidemokrasia mwezi ujao kama walivyokubaliana baada ya mapinduzi ya kijeshi.
Aidha, mamlaka ya mpito ya Guinea ilisema Jumatatu kwamba wao hawakuhusishwa na uamuzi wa jumuiya ya ECOWAS wa kuiwekea vikwazo Mali, na kwamba mpaka wao wa pamoja na Mali utabaki wazi. Ikumbukwe kwamba Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika -Magharibi Ecowas ilisimamisha uanachama wa Guinea mwezi Septemba baada ya mapinduzi yake ya kijeshi.