Urusi yazima shambulio jingine la droni mjini Moscow
23 Agosti 2023Moja kati ya ndege hizo ilipumbazwa kwa mifumo ya kielektroniki na kuanguka kwenye jengo moja katikati mwa Moscow. Na mbili nyingine ziliangushwa na mifumo ya usalama magharibi mwa mji huo mkuu.
Kutokana na mashambulizi hayo, viwanja vitatu vya ndege vya Moscow vilifungwa kwa muda, lakini tangu wakati huo huduma zimerejea tena. Hayo ni kulingana na vyombo vya habari vya serikali ya Urusi.
Mikanda ya video iliyotumwa na Gazeti la kila siku la Urusi la Izvestia kupitia mtandao wa Telegram, imeonesha gari la kuzima moto na magari mengine ya huduma za dharura yakiwa yamejipanga karibu na mtaa ambako mabaki ya droni yalianguka juu ya jengo la ghorofa.
Dirisha moja la jengo hilo la roshani kadhaa limeonekana limeharibika.
Meya wa Moscow asema hakuna aliyejeruhiwa kwenye shambulizi hilo
Watoa huduma za dharura walilikagua eneo la shughuli nyingi za biashara mjini Moscow. Hayo yamefahamishwa na meya wa mji huo, Sergei Sobyanini.
"Madirisha kadhaa kwenye majengo mawili jirani ya ghorofa tano yamepasuka," alisema afisa huyo. Hata hivyo ameongeza kuwa hakuna kifo wala majeruhi kwenye mkasa huo.
Katika wiki za karibuni mashambulizi mengine mawili ya droni ya Ukraine yalizimwa kwenye wilaya ya shughuli nyingi za mji wa Moscow. Kila moja lilisababisha uharibifu kidogo kwenye sehemu ya mbele ya majengo kadhaa marefu.
Urusi na Ukraine zimeshambuliana kwa kila upande kuilenga miji ya mwingine kwa ndege zisizo na rubani tangu kuzuka kwa vita vinavyoendelea.
Hujuma ya hii leo dhidi ya Moscow imefanywa saa kadhaa baada ya mamlaka za Ukraine kusema makombora ya Urusi yamevipiga vijiji viwili karibu na mji wa Ukraine wa Lyman, na kusababisha vifo vya watu watatu na kujeruhi wengine wawili.
Marekani yajitenga na mashambulizi ya Ukraine ndani ya ardhi ya Urusi
Wakati hayo yametokea, Marekani imesema haiishajihishi au kuiwezesha Ukraine kushambulia maeneo ya ndani mwa Urusi.
Hayo yameelezwa na msemaji wa Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Marekani baada ya Urusi kusema imedungua droni za Ukraine.
Afisa huyo amesema ni jukumu la Ukraine kuamua njia za kujilinda dhidi ya uvamizi wa Urusi na kusisitiza kuwa Moscow inaweza kumaliza vita hivyo muda wowote kwa kuondoa wanajeshi wake nchini Ukraine.