Urusi yawania kuizunguka Bakhmut
10 Januari 2023Kulingana na wizara ya ulinzi ya Uingereza, huenda vikosi vya Urusi na mawakala hao kwa sasa wanadhibiti eneo kubwa la mji huo wenye machimbo ya chumvi baada ya kujiimarisha katika kipindi cha siku nne sasa.
Soledar, mji uliopo katika mkoa wa Donbas unapatikana maili chache kutoka Bakhmut ambako wanajeshi kutoka pande zote wameshuhudia wenzao wengi wakipoteza maisha yao kutokana na mapigano makali kabisa kwenye eneo hilo.
Wizara ya ulinzi ya Uingereza imesema kwenye taarifa yake ya kiintelijensia kwamba mashambulizi yanayofanywa na wanajeshi wa Urusi katika mji wa Soledar ni moja ya mkakati wake wa kuizunguka Bakhmut kutokea upande wa kaskazini lakini pia yanalenga kuharibu ama mitambo ya mawasiliano ya Ukraine.
Soma Zaidi: Urusi yazidisha mashambulizi nchini Ukraine kwa lengo la kutwaa tena miji iliyoipoteza
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amesema kwenye hotuba yake kwa njia ya video jana usiku kwamba wanajeshi katika maeneo ya Bakhmut na Soledar wanaendelea kupambana licha ya uharibifu na mapigano makali.
"Vita vya kuipigania Donbas vinaendelea. Na ingawa wavamizi sasa wameelekeza nguvu zao zaidi kwenye mji wa Soledar, matokeo ya vita hivi vigumu na vya muda mrefu yatakuwa ukombozi wa Donbas yetu nzima. Ninawashukuru wanajeshi wetu wote wanaoilinda Bakhmut na kuonyesha kiwango cha juu zaidi na ustahimilivu. Shukrani kwa wapiganaji wote huko Soledar, ambao wanastahimili mashambulizi mapya na makali zaidi ya wavamizi."
Wizara ya ulinzi ya Urusi hata hivyo haijazungumzia chochote kuhusu Soledar ama Bakhmut wakati ilipozungumza na vyombo vya habari siku ya jana.
Maafisa wa Ukraine, wanaoongozwa na Jenerali Valery Zaluzhniy wameonya kwamba Urusi inaandaa wanajeshi wapya kwa ajili ya mashambulizi mapya dhidi ya Ukraine na pengine kwenye mji Kyiv. Hapo jana Zelenskiy alinukuliwa akiomba msaada zaidi wa silaha kutoka kwa washirika wake wa magharibi ili kukabiliana na wanajeshi wa Urusi na ikiwezekana kuwafukuza kabisa na kwa upande mwingine, akisisitizia juhudi za kidiplomasia.
Na huko Moscow, katibu wa Baraza la Usalama la kitaifa Nikolai Patrushev ambaye pia ni mshirika wa karibu wa Putin amesema mapema leo kwamba mataifa ya magharibu yanajaribu kwa namna mbalimbali kuismbaratisha Urusi na kuipoteza kabisa kwenye ramani ya kisiasa ulimwenguni. Patrushev ameliambia gazeti la Urusi la Argumenti i Fakti kwamba katikati ya ongezeko la vitisho vya kijeshi, ni muhimu kwa Urusi kuwa na majeshi na vikosi maalumu ili maadui wa Urusi wasijaribu hata kufikiria kwamba wanaweza kupambana nao.