Urusi yasimamishwa baraza la haki za Binaadamu la UN
8 Aprili 2022Hatua hiyo ya kusimamisha uanachama wa Urusi kwenye baraza la haki za binaadamu la Umoja wa mataifa inachukuliwa baada ya kundi la mataifa saba tajiri zaidi ulimwenguni, G7, Umoja wa Ulaya na Washington wakizidisha vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Moscow na hasa kufuatia picha za kutisha zilizosambaa hivi karibuni za miili ya watu wanaodaiwa kuuliwa na wanajeshi wa Urusi katika mji wa Bucha na Mariupol.
Soma Zaidi: Ukraine yailaumu Urusi kwa uhalifu wa kivita
Rais Joe Biden amesema visa vya watu kubakwa, kuteswa na kuuawa na katika baadhi ya matukio mengine miili yao kukatwakatwa ni ghadhabu dhidi ya ubinaadamu wao. Shirika la haki za binaadamu la Umoja wa Mataifa pia linasema ubakaji umekuwa ukitumika kama ngao ya vita nchini Ukraine.
Kyiv na washirika wake wa Magharibi wanavishutumu vikosi vya Urusi kwa kufanya uhalifu wa kivita kwa kuwalenga kwa makusudi raia nchini Ukraine. Urusi hata hivyo inakana shutuma hizo.
Moscow hata hivyo imepinga hatua hiyo ya kusimamishwa, kufuatia kura iliyopigwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA, ambayo imeiita kuwa isiyo ya haki na iliyochochewa kisiasa.
Nchini Ukraine kwenyewe, raia wameonywa kuondoka, wakati vikosi vya Urusi vikiaminika kujiandaa kufanya mashambulizi makubwa baada ya kuondoka Kiev na kaskazini mwa Ukraine. Jana Alhamisi, Meya wa Mariupol alitangaza kwamba watu 5,000 waliuawa kwenye mji huo.
Huko Washington wakati Marekani ikiangazia kuongeza mbinyo wa kiuchumi dhidi ya Urusi, baraza la Congress jana limepiga kura ya kuhitimisha mahusiano ya kawaida ya kibiashara na Moscow na kumruhusu rais Biden kuongeza ushuru wa bidhaa zinazotoka Urusi.
Uwezekano wa mazungumzo kati ya Urusi na Ukraine unazidi kufifia.
Huku hayo yakiendelea, uwezekano wa mazungumzo ya kumaliza vita vinavyoendelea Ukraine unazidi kufifia wakati Moscow ikiishutumu Ukraine kwa kubadilisha masharti yake tangu mazungumzo ya ana kwa ana ya mwezi uliopita yalipomalizika.
Waziri wa mambo ya nje wa Urusi, Sergei Lavrov amesema muswada wa makubaliano uliowasilishwa na Ukraine unaonyesha kwamba hawakuwa na nia ya kumaliza mapigano hayo lakini mshauri wa rais wa Ukraine Mykhailo Podolyak alijibu madai hayo akisema iwapo Moscow ilitaka kuonyesha utayari wa kuzungumza ilitakiwa kupunguza kiwango cha uchokozi.
Soma Zaidi: Urusi yasema mazungumzo ya amani na Ukraine yanaendelea
Zaidi ya watu milioni 11 wamekimbia makazi yao tangu Urusi ilipoivamia Ukraine Februari 24.
Huko Brussels, katibu mkuu wa Jumuiya ya kujihami ya NATO Jens Stoltenberg amesema jana kwamba muungano huo wa kijeshi unaongeza msaada wake kwa Ukraine pamoja na majirani zake kwa namna mbalimbali. Ametoa matamshi hayo wakati mawaziri wa mambo ya nje wa NATO pamoja na Ukraine, Umoja wa Ulaya, Finland, Sweden, Japan, New Zealand na Australia walipokuwa wakihitimisha mkutano wa siku mbili mjini Brussels.
Jana Alhamisi, waziri wa mambo ya nje Dymitro Kuleba aliyatolea mwito mataifa hayo akiwa Brussels kwenye mkutano wa mawaziri wa kigeni wa NATO kuisaidia kwa dharura Ukraine ikiwa ni pamoja na mifumo ya kujilinda, magari na ndege.
Mashirika: DW/AFPE