Urusi yaionya Uturuki dhidi ya kuiingilia Idlib
20 Februari 2020Urusi inayoungana na Iran kumsaidia rais Bashar al-Assad mara kadhaa imepigia kura ya turufu maazimio ya Umoja wa Mataifa ikiwa na matarajio ya ushindi kwa serikali ya Assad.
Wanadiplomasia kwenye Umoja wa Mataifa walisema hawakuweza kutoa taarifa kuhusiana na kumaliza mapigano nchini Syria kufuatia kura hizo za turufu za Urusi. Balozi wa Ufaransa kwenye Umoja huo Nicolas de Riviere aliwaambia waandishi wa habari kwamba "tulijaribu kwa kila hali kuandaa taarifa ya pamoja ya mwito wa kusitishwa uadui na kuruhusu misaada ya kiutu kuingia katika mkoa wa Idlib lakini kimsingi Urusi ilisema "Hapana" na hilo linaumiza sana."
Mjumbe wa Urusi kwenye Umoja wa mataifa Gier Pedersen, aidha amethibitisha kwamba hakukuwa na hatua zozote zilizofikiwa kwenye duru kadhaa za mazungumzo kati ya Uturuki na Urusi yaliyofanyika Ankara na Moscow. Mapema wiki hii Umoja wa Mataifa ulisema idadi kubwa ya watu waliopotea walikuwa ni wanawake na watoto. Ulionya kwamba watoto wadogo wanakufa kwa baridi kwa kuwa makambi ya misaada yalikuwa yamefurika.
Mwenyekiti wa tume ya uchunguzi nchini Syria, Paulo Pinheiro akiwa nchini Marekani amesema historia inajirudia nchini humo, na watoto wa Syria wanateseka wakati wanachama wenye mamlaka wakishindwa kutumia mamlaka yao kuzuia mashambulizi.
"Kukabiliwa kwa mashambulizi ya mara kwa mara na ukosefu wa usalama kumewaathiri sana watoto nchini Syria. Wavulana na wasichana wanaonyesha dalili za kiwewe, pamoja na matatizo ya kisaikolojia na kitabia. Pia wanakabiliwa na uchovu sugu na mfadhaiko mkali. Hii inatokea kwa watoto wote nchini Syria, pamoja na katika maeneo yanayodhibitiwa na Serikali." alisema Pinhero.
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan jana alisema mazungumzo na Moscow yaliyodumu kwa siku mbili yameshindwa kutoa matokeo yaliyotarajiwa na kuonya kwamba Uturuki huenda ikaanzisha mashambulizi nchini Syria isipokuwa tu Damascus itaamua kurudisha nyuma majeshi yake ifikapo mwishoni mwa mwezi. Alinukuliwa akisema kwenye hotuba kupitia televisheni kwamba "operesheni ya Idlib inakaribia, na wanahesabu siku na wanatoa maonyo ya mwisho."
Urusi ilijibu kitisho hicho kwa kuitaka Uturuki kupambana na magaidi katika mkoa wa Idlib badala ya kuitishia.
Hata hivyo, waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu amesema hii leo kwamba kumekuwepo na aina fulani ya makubaliano katika mazungumzo na Urusi kuhusu Idlib, ambako tayari Ankara imetishia kuivamia, ingawa amesema majadiliano hayo hayajafikia kiwango kilichotarajiwa.