1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Urusi na Ukraine waendelea kushambuliana

27 Machi 2024

Balozi wa Ukraine nchini Ujerumani Oleksii Makeiev amekanusha madai ya Urusi kwamba nchi yake ilihusika katika shambulio karibu na Moscow lililosababisha vifo vya watu wasiopungua 139.

https://p.dw.com/p/4eAga
Oleksii Makeiev, Balozi wa Ukraine kwa Ujerumani
Balozi wa Ukraine kwa Ujerumani, Oleksii Makeiev asema Urusi inajaribu kujiondoa kwenye lawama.Picha: Christoph Schmidt/dpa/picture alliance

Balozi huyo ametaja madai haya kama "ya kipuuzi." Haya yanajiri huku Ukraine ikidai kwamba Urusi imeishambulia kwa ndege zisizo na rubani. 

Akizungumza na kituo cha redio cha Ujerumani cha Deutschlandfunk balozi Makeiev amesema Urusi inajaribu kuishutumu Ukraine kwa ugaidi ili kujiondoa katika lawama na ufuatiliaji.

Soma pia: Ukraine yasema imeilenga meli ya kivita ya Urusi katika Bahari Nyeusi

Takriban watu 139 waliuawa na karibu 200 kujeruhiwa siku ya Ijumaa katika mashambulizi wakati watu wanne wenye silaha walipofyatua risasi kwenye ukumbi wa muziki wa Crocus City Hall. Hata hivyo kundi linalojiita Dola la Kiislam baadaye lilidai kuhusika na shambulio hilo.

Wasemaji wa Urusi wamezungumza kuhusu magaidi wenye itikadi kali za Kiislamu na kuashiria wangeweza kuchukua hatua kwa niaba ya Ukraine au wafuasi wake wa Magharibi.

Aidha katika mahojiano hayo Makeiev pia alipinga kauli za kiongozi wa chama cha Social Democrat (SPD) Rolf Mützenich la "kusitisha" vita akitolea mfano duru nyingi za mazungumzo na Urusi tangu 2014, ambayo Ujerumani pia ilihusika kwa kusema kwamba wito huo umesababisha vita kubwa zaidi barani Ulaya.

Mapambano yanaendelea

Vita vya Ukraine na Urusi
Waokoaji wakiendelea kutafuta waathiriwa baada ya shambulio la kombora la Urusi kwenye hoteli moja huko Kharkiv, Ukraine.Picha: State Emergency Service of Ukraine/REUTERS

Huku haya yakiri watu wanne wamejeruhiwa katika mashambulizi ya Urusi kwenye eneo la mashariki mwa Ukraine la Kharkiv wakati Moscow ikidai kudungua msururu wa mashambulizi ya roketi za Ukraine.

Kupitia mitandao ya kijamii, gavana wa eneo hilo Oleg Sinegubov amesema wanume watatu na mwanamke mmoja wote wa umri wa zaidi ya miaka 50 walijeruhiwa katika mashambulizi tofauti ya roketi na silaha nyingine kwenye miji na vijiji katika eneo hilo.

Soma pia: Urusi na Ukraine zaendelea kushambuliana kwa ndege za droni

Jeshi la Ukraine limesema kuwa vikosi vya Urusi vimevurumisha droni 13 zilizotengenezwa kutoka Iran usiku kucha kuelekea Ukraine na vikosi vyake vilifanikiwa kudungua droni 10 katika eneo la Kharkiv, eneo jirani la Sumy na karibu na mji mkuu Kyiv.

Urusi nayo imetangaza kwamba mifumo yake ya ulinzi, imedungua roketi 18 karibu na mji wa mpakani wa Belgorod ambao katika siku za hivi karibuni, umeshuhudia ongezeko la mashambulizi kutoka Ukraine.

Eneo la Kharkiv linapakana na Urusi na limekuwa likikabiliwa na mashambulizi ya mara kwa mara tangu Moscow ilipovamia Ukraine mnamo Februari 2022, huku mashambulio ya mabomu ya hivi majuzi yakiacha maelfu bila huduma ya umeme.

 

dpa//AFP