Urusi, Marekani zafanya mazungumzo kuhusu Ukraine
11 Januari 2022Baada ya mazungumzo ya zaidi ya saa saba mjini Geneva hapo jana, maafisa wa Urusi na Marekani wote walikubaliana kuendelea kuzungumza, ijapokuwa hakukuwa na ishara ya kuwepo na mafanikio makubwa.
Mkutano huo wenye umuhimu mkubwa kwa kila upande ulikuja wakati kukiwa na wasiwasi kuwa Urusi inapanga kuivamia Ukraine, ambayo ni jirani yake anayeegemea nchi za Magharibi.
Soma pia: NATO: Uwezekano wa kufikiwa makubaliano na Urusi ni mdogo
Moscow inataka hakikisho kutoka Washington na washirika wake wa NATO, ambao nao wametishia vikwazo vikali iwapo kutatokea shambulizi lolote. Naibu Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Urusi Sergei Ryabkov amesema alimhakikishia mwenzake wa Marekani Wendy Sherman, kuwa hofu waliyo nayo haina msingi. "Kwetu sisi ni lazima kabisa kuhakikisha kuwa Ukraine kamwe, kamwe haitakuwa mwanachama wa NATO. Ni suala la usalama wa kitaifa kwa Urusi."
Sherman alisema Urusi haikutoa ushahidi kuwa haitoivamia Ukraine, au ufafanuzi wowote wa kwa nini imepeleka vikosi vyake kwenye mpaka wa Ukraine. Waziri huyo pia alisisitiza kuwa baadhi ya masharti ya Urusi kimsingi hayawezekani kamwe ikiwemo kuipiga marufuku Jumuiya ya Kujihami ya NATO kuongeza wanachama wa upande wa mashariki. "Rudisheni askari kambini au mutuambie ni mazoezi gani yanaendelea na yana madhumuni gani. Hilo haliko wazi hata kidogo. Kwa kawaida mtu hapeleki tu askari laki moja kwenye mpaka."
Mazungumzo ya jana yamezindua wiki ya diplomasia kati ya Urusi na nchini za Magharibi. Mkutano wa Baraza la NATO na Urusi utafanyika kesho mjini Brussels, kisha baraza la kudumu la Shirika la Usalama na Ushirikiano Ulaya – OSCE litakutana Vienna Alhamisi huku suala Ukraine likitarajiwa kutawala.
Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg amesema jana kuwa muungano huo wa kijeshi utaionya Urusi kuhusu gharama kubwa zitakazotokana na uvamizi.
Stoltenberg amesema kabla ya mazungumzo na Olga Stefanishyna, mmoja wa manaibu waziri wakuu wanne wa Ukraine kuwa anatumai kutakuwa na makubaliano ya kuanzisha mchakato wa mikutano ya mazungumzo ya kidiplomasia
Soma pia: Putin, Biden wazungumzia mzozo wa Ukraine
Hatua dhidi ya Urusi zinazozingatiwa ni pamoja na vikwazo dhidi ya watu wa karibu wa Rais Vladmir Putin, kuufuta mradi wenye utata wa bomba la Nord Stream 2 la gesi kutoka Urusi kwenda Ujerumani, na katika hatua mbaya Zaidi, kuvunja mahusiano ya Urusi na mfumo wa benki ulimwenguni.
afp, ap, reuters