Putin, Biden wazungumzia mzozo wa Ukraine
31 Desemba 2021Katika mazungumzo ya saa nzima siku ya Alkhamis (Disemba 30), Biden alimtaka Putin kuacha kuendeleza shughuli za kijeshi mpakani mwa Ukraine, kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu ya Marekani.
"Aliweka wazi kwamba Marekani na washirika wake watachukuwa hatua endapo Urusi itaivamia Ukraine," ilisema Ikulu ya White House.
Afisa mwengine wa Ikulu hiyo aliliambia shirika la habari la dpa baada ya mazungumzo hayo kwamba "uingiliaji kati wowote dhidi ya Ukraine utapelekea vikwazo dhidi ya Moscow na kutanuka kwa Jumuiya ya Kujihami ya NATO kwenye mataifa ya mashariki, ukiwemo msaada wa vifaa na kijeshi kwa Ukraine."
Hata hivyo, licha ya kuelezea kuridhika na mazungumzo hayo, Rais Putin alionya kwamba vikwazo vipya dhidi ya nchi yake vinatishia mpasuko mkubwa baina yao.
Putin amuonya Biden
Mshauri wa sera za nje wa Putin, Yury Ushakov, alisema Putin alimuonya Biden kuwa Moscow inahitaji matokeo chanya na kwamba mkutano ujao wa masuala ya usalama hautakuwa na maana yoyote.
Ushakov alisema mazungumzo hayo yalifanikiwa na yangeliweza kusababisha kuimarika kwa mahusiano kati ya pande hizo mbili.
Putin alionekana kuwa tayari kuridhia mambo mengi, ikiwa matakwa yake ya kuhakikishiwa usalama na NATO yaliyowasilishwa wiki mbili nyuma yangelitekelezwa.
Miongoni mwa yanayotakiwa na Moscow ni NATO kuacha kujitanuwa kwenye eneo la mashariki mwa Ulaya.
Kwa mujibu wa Ushakov, Urusi ilikuwa tayari kuzingatia yaliyotakiwa na "upande wa Marekani na washirika wetu kwenye mataifa ya Magharibi katika majadiliano."
Mkutano wa Januari 10
Biden na Putin walijadili kwa kina hisia za kila upande wakati mzozo ukizidi kufukuta baina ya Urusi na mataifa ya Magharibi kuhusiana na suala la Ukraine, wakilenga kusaka suluhisho la kidiplomasia kabla ya mkutano rasmi utakayofanyika Januari 10 mjini Geneva, ambao utazijumuisha pia NATO na Jumuiya ya Ushirikiano ya Mataifa ya Ulaya (OSCE).
Marekani inaituhumu Urusi kwa kujijenga kijeshi karibu na Ukraibe, huku Urusi ikiituhumu Ukraine kwa kuimarisha jeshi lake katika eneo la mashariki linalopakana nayo.
"Pande zote mbili zina wajibu maalum kwa usalama wa dunia na wa eneo hili," alisema Putin kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kremlin, iliyoongeza kuwa mataifa hayo mawili "yanaweza na yanalazimika kushirikiana pamoja mbele ya changamoto na vitisho dhidi ya ubinaadamu."