Urusi: Marekani inachochea mzozo wa Ukraine
24 Januari 2022Akizungumza leo Jumatatu, msemaji wa ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov amesema, uwezekano wa kuanza kwa mgogoro wa kijeshi mashariki mwa Ukraine kwa sasa ni mkubwa kuliko wakati wowote ule.
Peskov amesema Ukraine imepeleka wanajeshi karibu na mipaka ya mikoa iliyojitenga inayodhibitiwa na waasi wanaoiunga mkono Urusi jambo ambalo amesema linaashiria kuwa Ukraine inajiandaa kuwashambulia madai ambayo Ukraine imekuwa ikiyakanusha mara kadhaa sasa.
Kauli hiyo ya Peskov imetolewa muda mfupi baada ya Jumuiya ya kujihami ya NATO kusema hapo awali kuwa inawaweka tayari na kuimarisha jeshi lake mashariki mwa Ulaya kwa kuongeza meli za kivita ikiwa ni majibu kwa Urusi iliyopeleka wanajeshi wake kati ya mipaka yake na Ukraine. Hatua hiyo ya NATO imezidisha ishara kuwa mataifa ya Magharibi yanajiandaa kuikabili Urusi ikiwa itachukua hatua yoyote dhidi ya Ukraine. Urusi yenyewe, inakanusha kuwa haina mpango wowote wa kulivamia taifa hilo.
Akiunga mkono hatua zilizotangazwa na jumuiya hiyo, katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg amesema, wataendelea kuchukua hatua zote muhimu ili kuwalinda washirika wake ikiwemo ya kuimarisha majeshi katika eneo la mashariki la jumuiya hiyo.
Ukraine haitajibu vitendo vya uchukozi
Naye rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema, nchi yake haitajibu uchokozi na badala yake itaendelea kudumisha utulivu na uvumilivi sambamba na washirika wake. Zelensky amezitaka pia nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kuendelea kuungana dhidi ya Urusi.
Katika hatua nyingine, rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema halmashauri kuu ya umoja huo inapendekeza msaada wa dola bilioni 1.2 kwa Ukraine ambao unajumuisha mikopo ya dharura na ruzuku ili kushughulikia madhara yanayojitokeza kwa haraka kutokana na mvutano na Urusi. Von der Leyen amesema, anataraji kuwa wabunge wa Umoja wa Ulaya watapitisha msaada huo wa dharura haraka iwezekanavyo.