Familia za wafanyakazi wa ubalozi wa Marekani kuondola Kiev
24 Januari 2022Hatua hiyo ya Marekani inakuja mnamo wakati mawaziri wa mambo ya nje wanatafuta kuoanisha majibu yao na Marekani, wakati waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken akishiriki mkutano wa wenzanke wa Umoja wa Ulaya kwa njia ya vidio.
Blinken atawaarifu mawaziri hao juu ya mazungumzo yake siku ya Ijumaa na waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov mjini Geneva, ambako pande mbili zilikubaliana kuendelea kufanya kazi kutuliza wasiwasi lakini walishindwa kupata muafaka wa kupunguza mzozo unaozidi kufukuta.
Mataifa ya Magharibi yanaituhumu Moscow kwa kutishia uvamizi zaidi dhidi ya jirani yake anaelemea magharibi kwa kulundika zaidi ya wanajeshi 100,000 kwenye mpaka wake, lakini Ikulu ya Kremlin inasisitiza kuwa vikosi vyake haviko huko kwa ajili ya uvamizi.
Soma pia: Mkuu wa jeshi la majini Ujerumani ajiuzulu kutokana na matamshi kuhusu Putin, Crimea
Wakati hali ya wasiwasi ikiongeza, Marekani imeidhinisha Jumapili uondokaji wa hiari wa watumishi wasio muhimu wa ubalozi wake na kuwahimiza raia wake katika taifa hilo la Ulaya Mashariki kuzingatia kuondoka sasa, kabla ya kile ilichokiita hatua za kijeshi za Urusi.
Ajenda ya kuweka kiongozi kibaraka wa Urusi
Siku ya Jumamosi, wizara ya mambo ya nje ya Uingereza ilidai Urusi ilikuwa inatafuta kuweka kibaraka wake katika uongozi nchini Ukraine, madai ambayo Urusi iliyataja kuwa upotoshaji.
Marekani imeongoza juhudi za kidiplomasia kumshawishi rais Urusi Vladmir Putin kutoishambulia Ukraine na kuwaongoza washirika wake kuandaa adhabu kubwa za kiuchumi dhidi ya Moscow iwapo itachukuwa hatua hiyo.
Blinken ameahidi kutoa majibu ya kimaandishi wiki hii kwa Moscow, baada ya kuainisha matakwa yake ya kiusalama ambayo yataizuwia Ukraine kujiunga na jumuiya ya kujihami NATO na kuondoa ushawishi wa Marekani katika eneo la Ulaya Mashariki.
Soma pia:Sintofahamu yaendelea kugubika mazungumzo kuhusu Ukraine
Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wanaokutana mjini Brussels wanataka kusikia maoni ya Marekani kuhusiana na mipango yake wakati ambapo Ulaya ikijihisi kuachwa nje ya mazungumzo kuhusu usalama wake yenyewe.
Marekani na Umoja wa Ulaya zimeitishia Moscow juu ya madhara makubwa iwapo itatuma vikosi vyake ndani ya Ukraine, lakini kupata muafaka juu ya hatua kali za kuimiza Urusi miongoni mwa mataifa 27 wanachama wa kanda hiyo imekuwa vigumu sana.
Vyanzo:rtre,afpe,dpa.