Urusi kuhamisha watu 10,000 kwa siku kutoka Kherson
19 Oktoba 2022Gavana huyo, Vladimir Saldo akizungumza kupitia jukwaa la mtandaoni la ''Soloviev Live'' amesema watu hao watahamishiwa kwenye ukingo wa kushoto wa mto Dnipro, ili kuwaweka mahali salama na kuliruhusu jeshi kufanya operesheni zake bila vizuizi.
Soma zaidi: Urusi yazidi kuishambulia Ukraine kwa Makombora ya angani
Saldo amesema ameendesha gari katikati mwa mkoa wa Kherson asubuhi ya leo, na kuongeza kuwa kwa kutazama kutoka mbali hakukuwa na dalili zozote za shinikizo. Hata hivyo, ameongeza kiongozi huo aliyewekwa na Urusi, alipoukaribi mto aliziona boti zilizojaa watu walio tayari kuuvuka mto, akisisitiza kuwa huko hali ilikuwa yenye mivutano mikubwa.
Kulingana na maelezo yake, mikoa kadhaa ya Urusi imeandaliwa kuwapokea wanaohamishwa kutoka Kherson, ikitarajiwa kuwa kiasi watu 10,000 watakuwa wakisafirishwa kila siku. Mnamo siku mbili zilizopita, tayari watu 5,000 waliuhama mkoa huo wenye mapigano.
Vikosi vya Urusi vyabanwa kwenye ukingo wa mto Dnipro
Duru zinaarifu kuwa katika kipindi cha wiki chache vikosi vya Urusi jimboni Kherson vimerudishwa nyuma kilomita kati ya 20 na 30, na kubanwa kwenye ukingo wa magharibi wa mto Dnipro wenye urefu wa km 2,200.
Huku hayo yakijiri upande wa kusini mashariki mwa Ukraine, maeneo mengine mengi ya nchi hiyo yanaendelea kukosa umeme kufuatia mashambulizi ya Urusi yaliyoilenga miundombinu ya nishati.
Soma zaidi: Ukraine yaomba vikwazo zaidi dhidi ya Iran
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amewasihi raia wa nchi hiyo kubana sana matumizi ya umeme.
Mfululizo wa mashambulizi ya makombora ya Urusi uliiharibu mitambo ya umeme na maji katika mji wa Enerhodar ulioko karibu na kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia, hayo yakiwa ni kwa mujibu wa meya wa mji huo, Dmytro Orlov.
Kiwanda kingine cha kufua umeme kiliharibiwa katika mji wa Kryvy Rih, na kuwaacha wakaazi wa miji na vijiji jirani katika giza.
Mbinu ya Putin kuwavunja moyo Waukraine
Wimbi hili la hivi karibuni la mashambulizi ya makombora na videge vidogo vinavyoharibika baada ya kupiga shabaha, linachukuliwa na wachambuzi kama mbinu mpya ya rais wa Urusi Vladimir Putin kuivunja ari ya raia wa Ukraine, ambayo imekuwa haitetereki tangu kuanza kwa uvamizi wa Urusi mwezi Februari.
Soma zaidi: Drones za kamikaze zaushambulia mji wa Kiev-Ukraine
Hapo jana Rais Zelenskiy wa Ukraine alisema kuwa karibu theluthi moja ya vituo vya nishati vya nchi yake viliharibiwa katika mashambulizi haya mapya ya Urusi yaliyoshika kasi tangu tarehe 10 Oktoba. Nchi za magharibi zimeahidi kuipa Ukraine msaada zaidi wa mifumo ya kuilinda anga yake.
Vyanzo: ape, afpe