Urusi yazidi kuishambulia Ukraine kwa Makombora ya angani
18 Oktoba 2022Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameyalaani mashambulizi hayo na kuyaita ya kigaidi dhidi ya raia wa taifa lake. Katika mtandao wake wa Telegram, rais Zelensky amesema adui anaweza kuyashambulia miji nchini humo lakini kamwe hatofanikiwa kuwagawa Waukraine.
Drones za kamikaze zaushambulia mji wa Kiev-Ukraine
Moja ya makombora yaliyovurumishwa mjini Kiev hii leo asubuhi yalilenga jengo la makaazi ya watu na kusababisha vifo vya watu wanne akiwemo mama mjamzito. Maafisa nchini humo wamesema watu kadhaa wameokolewa lakini bado kuna wengi wengine wanaoaminika kukwama huko.
soma zaidi: Ukraine yaomba vikwazo zaidi dhidi ya Iran
Kwa upande wake, waziri wa mambo ya ndani wa Ukraine Denys Monastyrskyy amesema Urusi ilirusha ndege 40 zisizo na rubani nchini humo, 5 kati ya hizo zilianguka mjini Kiev. Wizara ya Ulinzi imesema Moscow ililenga mifumo ya nishati na miundombinu katika mashambulizi yake ya angani na majini hii leo Jumanne.
Rais Zelensky aomba mifumo zaidi ya kujilinda na makombora
Tangu siku ya Jumapili jioni Ukraine imefanikiwa kuzuwiya droni 37 kushambulia nchini humo hii ikiwa ni kwa mujibu wa rais Zelensky aliyeendelea kuitolea mwito Jumuiya ya Magharibi kuipa mifumo zaidi ya kujilinda dhidi ya makombora ya angani.
"Tulifanikiwa kuharibu baadhi ya makombora na ndege zisizokuwa na rubani. Ndani ya masaa 12 kuanzia saa tatu asubuhi siku ya jumapili tulidungua droni 37. Lakini ili kuhakikisha ulinzi wa anga zetu na kupunguza ugaidi unaofanywa na Urusi tunahitaji zaidi mifumo ya kisasa ya kujilinda na makombora," alisema rais Zelensky
Makombora ya Urusi yaua watu 19 Ukraine
Kando na mashambulizi mjini Kiev kumeripotiwa pia mashambulizi mengine ya angani mjini Sumy, Dnipropetrovsk na Odessa. Mjini Sumi, watu watatu waliuwawa huku wengine tisa wakijeruhiwa.
Huduma za umeme na maji zimekatika katika miji kadhaa iliyoshambuliwa. Kinu kikubwa cha nyuklia cha Zaporizhzhya kinachodhibitiwa na Ukraine pia kwa mara nyengine tena kilikosa umeme ambao ni muhimu katika shughuli zake.
Azimio la Baraza Kuu la UN kulaani Urusi lapita kwa kura nyingi
Kampuni ya serikali ya Ukraine inayohusika na nishati ya nyuklia, Energo-atom imeishutumu Urusi kuihujumu Ukraine na dunia kwa ujumla kupitia mashambulizi hayo. Kampuni hiyo imetaka hatua za haraka kuchukuliwa ili kuilinda zaidi Ukraine na kinu hicho cha Zaporizhzhya ambacho ni kikubwa zaidi barani Ulaya.
Chanzo: dpa, afp