Urusi yaanzisha wimbi la mashambulizi ya "droni", Ukraine
19 Novemba 2023Mkuu wa utawala wa kijeshi mjini Kyiv Serhiy Popko amesema kupitia Telegram kwamba Urusi ilianzisha wimbi la mashambulizi ya droni kutokea pande tofauti huku wakibadilisha mara kwa mara, hatua iliyosababisha kutolewa kwa tahadhari za mashambulizi ya anga mara kadhaa kwenye jiji hilo.
Jeshi la anga la Ukraine limesema mifumo yake ya kujilinda angani ilidungua droni 15 kati ya 20 zilizorushwa na Urusi kuelekea miji ya Kyiv, Poltava na Cherkasy.
Popko amesema hakuna ripoti yoyote ya uharibifu mkubwa, vifo ama watu kujeruhiwa, na kuongeza kuwa karibu droni 10 ziliangukia Kyiv na kwenye viunga vyake.
Kyiv na Moscow zimeshambuliana usiku wa Jumamosi, ingawa pande zote mbili zimedai kuwa zilizuia mashambulizi mengi na hakuna athari iliyoripotiwa.