1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Urusi: Hatua ya kuipa Ukraine silaha zaidi yazidisha mzozo

21 Desemba 2022

Urusi imesema kuzidi kuipa Ukraine silaha kunazidisha mgogoro huo.

https://p.dw.com/p/4LHig
Russland l Präsident Putin, Sitzung des Vorstands des russischen Verteidigungsministeriums
Picha: Sergei Fadeichev/TASS/dpa/picture-alliance

Huku rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky akitarajiwa kukutana na rais wa Marekani Joe Biden nchini Marekani ambapo ataahidiwa silaha zaidi na mfumo wa ulinzi, Urusi imesema hatua ya kuiendelea kuipa Ukraine silaha inazidisha mzozo uliopo.

Akizungumza na waandishi wa habari, msemaji wa serikali ya Urusi Dmitry Peskov amesema bila shaka hatua ya kuendelea kuipa Ukraine silaha inazidisha mzozo.

"Upelekaji wa silaha kwa Ukraine unaendelea na kiwango cha silaha mbalimbali zinazotolewa kinaongezeka. Haya yote yanazidisha mgogoro. Hii haiendi vizuri kwa Ukraine,” amesema Peskov, alipokuwa akijibu swali la mwandishi habari kuhusu msimamo wa Urusi kuhusu mazungumzo ya amani.

Zelensky atembelea wanajeshi mstari wa mbele wa vita

Hiyo ndiyo ilikuwa kauli rasmi ya kwanza ya Urusi tangu ilipobainika kwamba Rais Zelensky anaelekea Marekani kukutana na Rais Biden, ambayo pia ndiyo ziara ya kwanza ya Zelensky inayofahamika tangu Urusi ilipoivamia nchi yake Februari 24.

Dmitry Peskov, msemaji wa rais wa Urusi
Dmitry Peskov, msemaji wa rais wa UrusiPicha: Elena Palm/ZUMAPRESS.com/picture alliance

Peskov pia alithibitisha kwamba Rais Vladimir Putin hatatoa hotuba ya kila mwaka kuhusu hali ya nchi mwaka huu. Peskov hakutoa sababu za uamuzi huo huku akisema tu ni kutokana na majukumu mengi yar ais.

Baadhi ya vyombo vya habari vya Urusi vimehusisha uamuzi wa Putin kutotoa hotuba ya hali ya nchi na vita vya Ukraine ambavyo Urusi imepoteza nguvu yake. Mapema mwaka huu, serikali ya Urusi pia ilifuta mkutano wa kila mwaka wa Putin na waandishi habari ambao tangu mwaka 2012 hufanyika mwezi Disemba.

White House: Ziara ya Zelensky kuonesha mshikamano wa nchi za Magharibi

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky atakuwa mgeni wa rais wa Marekani Joe Biden katika ikulu ya White House mjini Washington leo, ikiwa ni ziara ambayo ikulu ya Marekani imesema itatoa ujumbe wa mshikamano imara wa nchi za Magharibi.

Kulingana na White House, ziara ya Rais Volodymyr Zelensky nchini Marekani yalenga kutoa ujumbe wa mshikamano imara baina ya nchi za Magharibi
Kulingana na White House, ziara ya Rais Volodymyr Zelensky nchini Marekani yalenga kutoa ujumbe wa mshikamano imara baina ya nchi za MagharibiPicha: Ukrainian Presidential Press Office/AP/picture alliance

Zelensky anatarajiwa kupewa ahadi ya  msaada wa kijeshi wenye thamani ya dola bilioni 1.8, kusaidia nchi yake kujilinda dhidi ya mashambulizi ya Urusi.

Hali "mikoa mipya" ya Urusi ngumu sana - Putin

Msaada huo wa sasa wa Marekani utajumuisha pia mfumo wa ulinzi aina ya Patriot na makombora. Hayo yalisemwa Jumanne na afisa mmoja wa Marekani.

Ziara hiyo iliyopangwa kisiri imekuja wakati mmoja na siku ambayo rais wa Urusi Vladimir Putin amepanga kukutana na wakuu wa kijeshi kutathmini mzozo wa Ukraine na malengo yao ya mwaka ujao. Kremlin imesema kutakuwa na hotuba muhimu.

Diplomasia ya Urusi: Dmitry Medvedev akutana na Rais Xi Jinping

Zelensky akizuru Marekani, Urusi nayo ilihusika na diplomasia ya viwango vya juu.

Vikosi vya Urusi vimedaiwa kuendeleza mashambulizi siku ya Jumatano katika mji wa Nikopol.
Vikosi vya Urusi vimedaiwa kuendeleza mashambulizi siku ya Jumatano katika mji wa Nikopol. Picha: Libkos/AP/dpa/picture alliance

Naibu mwenyekiti wa baraza lake la Usalama Dmitry Medvedev alizuru China na kukutana na rais Xi Jinping. Rais huyo wa zamani wa Urusi alisema walijadiliana kuhusu ushirikiano wa kimkakati baina ya nchi zao na vilevile mgogoro wa Ukraine.

Hayo yakijiri, nchini Ukraine vikosi vya Urusi viliendeleza mashambulizi  ya makombora katika maeneo yenye wakaazi wengi. Miongoni mwa maeneo Urusi imeshambulia ni Nikopol, lililoko kusini mashariki mwa Ukraine. Gavana wa jimbo hilo Valentyn Reznichenko amethibitisha hayo kupitia ukurasa wake wa Telegram.

Ikulu ya rais nchini Ukraine imeripoti mapema leo kwamba raia watano wameuawa na wengine 17 wamejeruhiwa kufuatia mashambulizi ya Urusi tangu Jumanne.

Vyanzo: (APE, AFPE)