Hali "mikoa mipya" ya Urusi ngumu sana - Putin
20 Desemba 2022Akizungumza na vyombo vya usalama siku ya Jumanne (Disemba 20) mjini Moscow, Rais Putin alisema hali kwenye Jamhuri za Watu wa Donetsk na Lugansk, mikoa ya Kherson na Zaporizhzhia ni mbaya sana.
Akiwalenga makhsusi kabisa maafisa wake wanaofanya kazi kwenye maeneo hayo anayoyaita "mikoa mipya ya Urusi."
"Watu wanaoishi huko, raia wa Urusi, wanawategemeeni nyinyi, wanategemea ulinzi wenu. Idadi kubwa ya vikosi inahitajika kuendeleza operesheni za kiusalama na kiujasusi ili kuyadhibiti mashirika ya kijasusi ya kigeni, kuwatambuwa wasaliti, wapelelezi, na wanaotuhujumu." Alisema kiongozi huyo wa Urusi.
Mnamo mwezi Septemba, Putin alitangaza rasmi kuyachukuwa majimbo manne yaliyoko kusini na mashariki mwa Ukraine baada ya watawala wa majimbo hayo wanaoiunga mkono Moscow kuitisha kile walichokiita "kura ya maoni", ambayo ililaaniwa vikali na Kiev na washirika wake wa Magharibi.
Hata hivyo, vikosi vya Urusi havijawahi kuwa na udhibiti kamili wa jimbo lolote kati yao na mwezi Novemba vililazimika kuukimbia mji mkuu wa mkoa wa Kherson baada ya miezi kadhaa ya kukabiliwa na mashambulizi ya wanajeshi wa Ukraine.
Iran yakabiliana na Marekani kikao cha Umoja wa Mataifa
Kufuatia kushindwa kwenye vita vyake vya ardhini, sasa Moscow imebadilisha mkakati na kugeukia mashambulizi ya angani inayolenga miundombinu ya kijeshi na nishati ya Ukraine.
Siku ya Jumatatu (Disemba 19), Marekani na washirika wake walishambuliana kwa maneno na Iran na mshirika wake, Urusi, juu ya tuhuma kwamba Tehran inaipatia Moscow ndege zisizo rubani ambazo zimekuwa zikitumika kuishambulia Ukraine.
Katika kikao kilichoitishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kujadili azimio lililoridhia mkataba wa nyuklia kati ya Iran na mataifa sita yenye nguvu duniani, Marekani ilifika umbali wa kumkosowa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa kunywea kutokana na vitisho vya Urusi na matokeo yake kushindwa kuamuru uchunguzi juu ya madai hayo.
Iran, Urusi zakanusha
Balozi wa Iran kwenye Umoja huo, Amir Saeid Iravani, alisema kwamba tuhuma kuwa nchi yake imevunja makubaliano hayo ya mwaka 2015 kwa kutuma ndege hizo kwa Urusi hazina msingi.
"Masharti yote ya kutuma silaha kutoka na kuingia nchini Iran yalikoma mwezi Oktoba 2020." Alisema Balozi Iravani, aliyeongeza kuwa Marekani na washirika wake wanatumia suala hilo kukwepa ukweli kwamba wao wamekuwa wakiipatia silaha Ukrainekuishambulia Urusi.
Kwa upande wake, Balozi wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa, Vassily Nebenzia, alikanusha vikali nchi yake kutumia ndege kutoka Iran kwenye kampeni yake ya kijeshi nchini Ukraine, akisema kuwa hakuna ndege hata moja inayotumika huko isiyotoka Urusi.
Naibu Balozi wa Marekani kwenye Umoja huo, Robert Wood, alisisitiza kwamba kuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha madai yao, akirejelea hoja ya mataifa ya Magharibi kwamba "Iran hairuhusiwi kisheria kuchukuwa uamuzi kama huo bila idhini ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa."