1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ursula von der Leyen afanya ziara nchini Senegal

Josephat Charo
9 Februari 2022

Rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen leo (09.02.2022) anatarajiwa kuwasili mjini Dakar nchini Senegal.

https://p.dw.com/p/46ieA
Frankreich Paris | EU-Kommissionspräsidentin | Ursula von der Leyen
Picha: Michel Euler/Pool/REUTERS

Uthabiti wa bara la Afrika na haja ya kuepusha machafuko na kuyumba kwa mifumo ya kisiasa kunakosababishwa na matumizi ya nguvu ni masuala ya kipaumbele katika ajenda ya mkutano huo wa kilele. Huku China na Urusi zikifanya juhudi kubwa za kuzishawishi na kuzivutia nchi masikini za Afrika na mikopo na kuzisaidia na msaada wa usalama, Von der Leyen amesema mshirika wa bara la Afrika wa kuaminika na kutegemewa zaidi ni Ulaya. Kila mwaka Umoja wa Ulaya huwekeza euro bilioni 20 katika misaada ya fedha kwa bara hilo pamoja na mikopo na dhamana.

Katika mahojiano na shirika la habari la Ufaransa, AFP kabla kwenda Senegal Von der Leyen alisema ataitumia ziara yake hiyo kuzindua mpango wa kwanza kwa ajili ya Afrika katika mpango mpya wa uwekezaji uliopewa jina la Global Gateway, Lango Kuu la Kimataifa. Mradi huo kati ya Afrika na Ulaya ambao unaonekana kuwa jibu kwa mradi mkubwa wa ujenzi wa miundombinu ya barabara wa China, unalenga kufanya uwekezaji wa thamani ya hadi euro bilioni 300 katika ujenzi wa miundombinu ya umma na ya kibinafsi kote ulimwenguni.

Changamoto za uwekezaji zaifanya Afrika kuwa tegemezi

Von der Leyen  amedokeza kuwa fursa za uwekezaji barani Afrika mara nyingi zina gharama zinazojificha, akisema gharama za kifedha, kisiasa, kimazingira na kijamii mara nyingine huwa kubwa mno. Hali hii mara nyingi husababisha utegemezi zaidi badala ya ushirikiano halisi. Rais huyo wa kamisheni ya Umoja wa Ulaya amesema anaamini masuala haya hayatawaondoa kutoka malengo yao ya mkutano wa kilele badala yake ni viashiria vya wazi vya umuhimu wa kushirikiana pamoja kuleta mabadiliko nyanjani na kuyaboresha maisha ya watu, kuimarisha utawala na kutoa fursa nzuri zaidi.

Senegal Coronavirus l Präsident Macky Sall
Macky Sall, rais wa SenegalPicha: Ludovic Marin/Pool/REUTERS

Ameueleza mkutano kati ya Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika kuwa na umuhimu mkubwa akisema anauona kama fursa ya kuimarisha ushirikiano ambao Afrika na Ulaya zinauhitaji, kwa sababu pande hizo mbili zinahitaji kufanya kazi kwa karibu zaidi kuzitafutia ufumbuzi changamoto za leo - kama athari halisi za mabadiliko ya tabia nchi au afya. Pia amesema wanahitaji kuandaa ajenda yao chanya, itakayojikita katika maendeleo ya pamoja na ukuaji endelevu unaowanufaisha watu moja kwa moja.

Von der Leyen amesema hili ndilo lengo kubwa la mradi wa Global Gateway, atakaouzindua mjini Dakar na mkutano kati ya Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika unatakiwa kujadili hatua za kwanza za kimkakati katika ujenzi wa miundombinu, kuongeza thamani bidhaa, kuendeleza sekta binafsi, mafunzo ya stadi za maisha na afya.

Kesho Alhamisi Von der Leyen atakutana na rais wa Senegal, Macky Sall, ambaye ndiye mwenyekiti wa Umoja wa Afrika.

afp