1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani Uturuki wataka uchaguzi wa 2018 ufutiliwe mbali

Amina Abubakar Daniel Gakuba
8 Mei 2019

Chama kikuu cha upinzani Uturuki CHP kimeitolea mwito baraza kuu la uchaguzi, kufutilia mbali uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka uliopita na uchaguzi wa serikali za mitaa kufuatia tangazo la kurudia uchaguzi wa Meya.

https://p.dw.com/p/3IBRi
Türkei, Istanbul: Bürgermeister Ekrem Imamoglu hält Ansprache
Picha: Getty Images/B. Kara

Siku ya Jumatatu baraza hilo kuu la uchaguzi YSK  liliamuru kufanyika tena kwa uchaguzi wa Meya uliompa ushindi Ekrem Imamoglu kutoka chama cha upinzani cha Republican Peoples Party CHP.

Baraza hilo la uchaguzi limesema matukio ya udanganyifu yaliyotajwa na chama cha rais Recep Tayyip Erdogan AKP ndio yaliyopelekea uchaguzi huo kuamuliwa kufanyika tena. 

"Kama unapinga madaraka ya bwana Ekrem Imamoglu, na kama unasimamia uamuzi wako basi unapaswa pia kupinga madaraka ya rais Erdogan," alisema Naibu mkuu wa chama cha upinzani CHP Muharrem Erkek akizungumza na waandishi habari mjini Ankara, Uturuki.

Türkei |  Recep Tayyip Erdogan in Ankara
Picha: picture-alliance/dpa/AP Photo/Pool/Presidential Press Service

Imamoglu alikuwa amemshinda mgombea wa chama tawala na waziri mkuu wa zamani Binali Yildirim Istanbul kwa asilimia ndogo tu hii ikiwa ni kulingana na matokeo ya mwanzo yaliyotolewa.

Erkek amesema sheria hizo hizo, kanuni hizo hizo, vituo vya kupigia kura hivyo hivyo  na mazingira sawa na yaliyotajwa ndio yaliyokuwepo pia katika chaguzi zote, akitaka uchaguzi wa rais na ule wa wabunge uliofanyika mwaka uliopita mwezi Juni ufutiliwe mbali.

Upinzani: Kama madaraka ya Ekrem hayatatambuliwa na ya Erdogan yasitambuliwe 

Erdogan alichukua tena nafasi yake baada ya kushinda uchaguzi huo mwaka uliopita. Tarehe 31 mwezi Machi wapiga kura walipiga kura zao kumchagua meya wa mji huo, meya wa wilaya pamoja na wajumbe wa baraza la mameya na viongozi wa maeneo jirani. Lakini Baraza la uchaguzi limeamua kufutilia mbali uchaguzi wa meya pekee.

Huku hayo yakiarifiwa rais wa zamani na waziri wa zamani wote wanachama wa chama tawala cha AKP wameukosoa uamuzi wa baraza la uchaguzi kuamuru tena kufanyika kwa uchaguzi wa kiti cha umeya wa Instanbul hii ikiwa ni kitu ambacho hakikutarajiwa kutoka kwa upande wa chama tawala chake rais Erdogan.

Vyanzo: AFP/Reuters