1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Hakuna demokrasia Uturuki

7 Mei 2019

Kuna utata nchini Uturuki baina ya chama tawala cha AKP na chama cha CHP kufuatia kufutiliwa mbali kwa ushindi wa Meya wa Istanbul katika uchaguzi uliofanywa mwezi Machi na uchaguzi mpya kupangiwa mwezi Juni.

https://p.dw.com/p/3I3nM
Türkei, Istanbul: Bürgermeister Ekrem Imamoglu hält Ansprache
Meya Ekrem Imamoglu Picha: picture-alliance/dpa/L. Pitarakis

Mwandishi wa DW Erkan Arikan, katika uchambuzi wake anasema, matokeo ya uchaguzi huo mpya hayajalishi kwani demokrasia nchini humo tayari imeshapoteza.

Kushindwa ni jambo ambalo halipo kabisa kwa Rais Recep Tayyip Erdogan hasa inapokuja katika mji wa Istanbul. Baada ya uchaguzi wa Meya kwisha Machi 31, ilikuwa wazi kwamba mambo yataendelea katika mji huo mkuu. Hata baada ya mshindi wa uchaguzi Ekrem Imamoglu kutoka chama cha upinzani cha CHP kukabidhiwa cheti cha ushindi wa Meya wa mji huo wenye idadi ya watu milioni 15, chama cha AKP na Rais Erdogan walifanya kila hila kuhakikisha kuwa hawapotezi nafasi hiyo hapo Istanbul.

Baraza Kuu la Uchaguzi Uturuki haliusikizi upinzani

Kwanza ilisemekana kura zihesabiwe upya katika wilaya za mji huo kisha baadae ikadaiwa kulikuwa na makosa katika karatasi za kupigia kura. Na sasa inasemekana kwamba wakuu katika uchaguzi huo hawakuwa maafisa wa kitaifa. La kushangaza lakini ni kwamba kiasi kikubwa cha maafisa wa uchaguzi walikuwa wa chama cha AKP.

Türkei, Istanbul: Bürgermeister Ekrem Imamoglu hält Ansprache
Wafuasi wa Meya Ekrem ImamogluPicha: Reuters/M. Sezer

Hata iwapo kulikuwa na mambo zaidi ya kutokubaliana katika chaguzi zilizopita, Baraza Kuu la Uchaguzi nchini humo lilikuwa siku zote linayakataa malalamiko ya upinzani. Lakini sasa mambo ni tofauti. Suala moja lakini ni muhimu kuzingatia - uamuzi wa Baraza Kuu la Uchaguzi ndiyo msumari wa mwisho katika jeneza la demokrasia nchini Uturuki.

Ila sasa kuna maswali, kwanini Baraza Kuu la Uchaguzi linayatambua malalamiko ya chama cha AKP? Kwanini uamuzi uliahirishwa mara tatu? Kurudiwa kwa uchaguzi Istanbul kunaliathiri vipi soko la hisa? Hakuna majibu, kuna uvumi tu kwamba hata Baraza Kuu la Uchaguzi halikuweza kuhimili shinikizo la Rais Erdogan. Ni vyema kufahamu kwamba uamuzi wa baraza hilo ndio wa mwisho, hauwezi kubatilishwa.

Wachumi wanasema sarafu ya Uturuki itashuka iwapo uchaguzi utafanyika tena

Kuchagua siku ya Jumatatu kutoa uamuzi ilikuwa ni mbinu ya kijanja kwa kuwa ni siku ya kwanza ya mwezi wa Ramadhan na hakuna ambaye angejitokeza kuandamana.

Türkei |  Recep Tayyip Erdogan in Ankara
Rais Recep Tayyip ErdoganPicha: picture-alliance/dpa/AP Photo/Pool/Presidential Press Service

Wataalam wa uchumi hivi majuzi tayari walitabiri kwamba sarafu ya Uturuki ya lira itapoteza thamani pakubwa dhidi ya yuro na dola iwapo uchaguzi wa Istanbul utarudiwa.

Lakini kitu kimoja kiko wazi, haijalishi uchaguzi utafanyika kwa njia gani hiyo Juni 23, demokrasia nchini Uturuki imeshashindwa.

Mwandishi: Erkan Arikan

Tafsiri: Jacob Safari

Mhariri: Mohammed Khelef