Upinzani Kongo wataka wachunguzi kutoka nje mauaji ya Okende
17 Julai 2023Waziri huyo wa zamani wa Uchukuzi aliuawa baada ya kutekwa nyara Jumatano iliyopita mjini Kinshasa.
Mwili wake uliojaa matundu ya risasi ulipatikana Alhamisi na hapo hapo uchunguzi ulianzishwa.
Serikali ya nchi hiyo imeeleza kuwa wachunguzi wa Kongo watashirikiana na wale wenzao kutoka nchi rafiki.
Soma pia:Waziri wa zamani DRC aliehamia upinzani akutwa amekufa
Katika uchunguzi huo, washukiwa wawili tayari wako kizuizini wakihojiwa, nao ni polisi mlinzi wa Chérubin Okende pamoja na dereva wake.
Lakini serikali imeomba msaada wa wachunguzi kutoka Ubelgiji na Afrika Kusini ili kutafuta ushahidi wa zaidi wa kimazingira ambapo mbunge huyo alitekwa nyara na hatimae kuuawa.
EPR:Tutafadhili wachunguzi zaidi kutoka nje
Chama cha Ensemble pour la République ambacho Okende alikuwa ni mwanachama hai, kinataka kufadhili wataalamu wa nje, kinataka Ufaransa, Uingereza na Marekani kushirikishwa katika uchunguzi huo ili kuepusha upotoshaji wowote wa ushahidi.
Francis Kalombo, naibu msemaji wa chama hicho alisema kuna haja ya kuhusisha wachunuzi zaidi kutoka mataifa ya Ufaransa, Marekani na hata Uingereza.
"Ensemble pour la République iko tayari kufadhili utaalamu ambao serikali ya Kongo inauhitaji."
Aliongeza kwamba hivi tayari wamefanya mawasiliano na baadhi ya makampuni ya kisheria nchini Marekani ili satelaiti za Marekani kufuatilia njia gari iliyopitia.
Soma pia:Rais wa zamani wa Kongo Kabila awataka wafuasi kupinga udikteta
Wachunguzi wa kigeni hata hivyo watalazimika kufanya kazi kwa ushirikiano na wenzao wa Kongo chini ya uratibu wa ofisi ya mwendesha mashtaka mkuu wa hapa nyumbani.
Yaani, kufuatia jinsi Kongo haina teknolojia muhimu, utaalamu wa kimataifa unahitajika ili kutambua jinsi mwisho wa maisha ya Chérubin Okende ulivyokuwa.
Ndivyo alivyoeleza Carlos Mupili, mtaalamu wa sheria ya uchunguzi wa kidijitali:
Alisema Kongo bado ipo nyuma katika teknolojia ya kidijitali,hivyo ushirikiano na wachunguzi wa nje ni mhimu.
"Ukweli ni kwamba katika uhalifu huo wengi wanashukia serikali."
Aliongeza kwamba jambo hilo huenda likaathidi sehemu fulani ya zoezi la uchaguzi hapo mwezi Desemba, hasa katika suala zima la matokeo ya uchaguzi.
Katika kuwatia katika mikono ya sheria wahusika katika mauaji ya mubunge huyo wa kitaifa, mahakama ya kikatiba tayari imetoa mwito kwa yeyote mwenye ushahidi utakaofanikisha haki dhidi ya muathirika wa mauaji hayo.