1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Aliyekuwa Rais Kongo Kabila awataka wafuasi kupinga udikteta

Jean Noel Bamweze19 Juni 2023

Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Joseph Kabila ametoa wito kwa wafuasi wake kupinga kile anachokielezea kuwa udikteta ambao tayari umeikumba nchi hiyo

https://p.dw.com/p/4SkcS
DR Kongo Ex-Präsident Joseph Kabila
Picha: picture-alliance/AP/J. Delay

Kabila alikumbusha kwamba yeye na muungano wake wa kisiasa hawatashiriki mchakato wa uchaguzi kabla mchakato huo kutimiza masharti ya uchaguzi bora. Upande wake, Denis Kadima, Kiongozi wa tume huru ya uchaguzi, ametoa wito kwa mchango wa wote ili kufikilia  mchakato wa uchaguzi utakaoaminika.

Soma pia: Upinzani DR Kongo wamtaka Tshisekedi kuacha kuwachokoza

Joseph Kabila alikuwa amebaki  kimya kwa muda mrefu baada ya kuacha madaraka Januari 2019 kwa mrithi wake Felix Tshisekedi. Kimya hicho kiliwafanya wengi kufikiria kwamba raïs huyo wa zamani amestaafu kisiasa. Lakini wikendi iliyopita, miezi sita kabla ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi wa Desemba mwaka huu, Kabila alikutana na viongozi wa FCC ambayo ni muungano wa vyama vinavyomuunga mkono na kuwaahidi kuwa atazidisha mikutano na wale ambao wamebaki waaminifu kwake. Miongoni mwa wale walioshiriki  mkutano huo ni Ferdinand Kambere, Naibu Katibu Mkuu wa PPRD, chama cha Joseph Kabila.

DR Kongo Der Präsident der Demokratischen Republik Kongo Félix Tshisekedi
Rais Tshisekedi atawania urais kwa muhula wa piliPicha: Giscard Kusema, der Kommunikationsmanager der Kongo-Präsidentschaft

"Lengo la mkutano huo lilikuwa ni kumhakikishia kila mtu kwamba Kabila bado yupo na kwamba wale wanaofikiri kuwa ukimya wake ulimaanisha kustaafu kisiasa wamedanganyika. Alikuwa amejipa tu muda ili kukabiliana na haya mapinduzi ya kitaasisi na pia kuwaacha raia wenyewe kutathmini tabia ya kila mtu. Kwa hivyo, aligusia hali hii ambayo nchi inapitia."

Soma pia: Kongo yaandikisha wapiga kura

Joseph Kabila anadai masharti yote ya kufanyika uchaguzi bora kutimizwa na bila hayo, basi yeye na wafuasi wake hawatashiriki mchakato wa uchaguzi huo. Upande wake tume ya uchaguzi, CENI, imesema kwamba imedhamiria kuwatolea Wakongo mchakato wa uchaguzi ulio bora na wa kuaminika. Ndivyo alivyosisitiza jumamosi, Dénis Kadima, mwenyekiti wa CENI,  wakati wa mkutano na viongozi wa tume hiyo pamoja na wawakilishi wa washirika wa CENI. 

"Nchi lazima isonge mbele. Hatuwezi kuendelea kufanya  uchaguzi tukipoteza ubora. Badala yake, lazima kujifunza kutokana na makosa ya hapo awali. Kumekuwa na kelele nyingi kuhusu mambo fulani katika michakato ya zamani, lakini pia kulikuwa na mambo mazuri. Tunaendelesha  yaliyofanyika vizuri na pale ambapo kulikuwa na makosa hatutayarudia. Hii ni ahadi tunayowatolea."

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inajiandaa kufanya chaguzi nne Desemba 20. Nazo ni uchaguzi wa rais, ule wa wabunge wa kitaifa na wa mikoa, pamoja na chaguzi za manispaa.

Jean Noël Ba-Mweze, Kinshasa