UNRWA: Lita 120,000 za mafuta zahitajika Gaza kila siku
18 Novemba 2023Akizungumza na DW kutoka mji mkuu wa Jordan Amman, Touma amesema hawajaweza kuendelea kutoa msaada kwa sababu ya ukosefu wa mafuta na pia kutokana na kukatika kwa huduma za mawasiliano. Amethibitisha kuwa hakuna mafuta yaliyofikishwa Gaza Jana Ijumaa. Baraza la Mawaziri la Israel linaloshughulika na vita hivyo liliidhinisha kuruhusu malori mawili yaliyobeba mafuta kuingia Gaza kutokea Misri kila siku.
Soma pia:Mawasiliano Gaza yapungua kwa siku ya pili mtawalia
Hata hivyo kampuni za mawasiliano ya simu za Paltel na Jawwal zilisema kuwa huduma za simu na intanet zimerejeshwa kwa sehemu katika Ukanda wa Gaza. Zimesema hatua hiyo ilijiri baada ya kuingizwa kwa kiasi Fulani cha mafuta kupitia shirika la UNRWA. Shirika la Habari la AFP liliripoti kuwa maafisa wa mpaka wa Gaza walisema lita 17,000 za mafuta zilifikishwa katika ukanda huo jana usiku.
Idadi ya vifo Gaza yafikia 12,000, Wizara ya Afya Gaza yasema
Wizara ya afya ya Gaza inayoendeshwa na kundi la Hamas imesema kuwa idadi ya vifo katika Ukanda wa Gaza kufuatia operesheni ya kijeshi ya Israel, inayoendelea tangu mashambulizi ya kigaidi ya Oktoba 7 imefikia watu 12,000. Idadi hiyo ni Pamoja na karibu Watoto 5,000 na wanawake 3,000. Wizara hiyo imesema watu wengine 30,000 wamejeruhiwa.
Awali, Wizara hiyo ya Afya ilisema isingeweza kutoa idadi kamili ya vifo kutokana na ugumu wa kuiondoa miili kutokana na mapigano makali.
Soma pia:Uhaba wa mafuta wasitisha huduma za kibinaadamu Gaza
Wanajeshi wa Israel waliendelea na msako wao kwa siku ya tatu jana Ijumaa katika hospitali ya Al-Shifa, wakitafuta kile wanachosema ni kituo cha kamandi ya Hamas ambacho makamanda wao wanasema kimefichwa katika mahandaki yaliyoko chini ya hospitali hiyo. Wanamgambo hao na wakurugenzi wakuu wa hospitali hiyo wanakanusha kuwepo kwa kituo cha aina hiyo mahali hapo.
Scholz ashughulikia ‘tofauti' na Erdogan kuhusu Israel
Mjini Berlin, katika kikao cha pamoja cha waandishi habari jana usiku, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz alisisitiza kuwa haki ya Israel ya kujilinda haipaswi kutiliwa shaka. Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, wakati huo huo, aliendeleza ukosoaji wake mkali wa operesheni ya Israel inayoendelea Gaza akilaani kushambuliwa hospitali na kuwauwa watoto. Akizungumza na waandishi Habari wakati wa ziara ya Erdogan mjini Berlin, Scholz amesema sio siri kuwa yeye na rais wa Uturuki wana mitazamo tofauti kabisa kuhusu mzozo huo wa sasa.
Soma pia:Ujerumani inaangazia kusaka suluhu ya uhusiano kati yake na Uturuki ambao mara zote umekuwa mgumu
Kiongozi huyo wa Ujerumani amesema hakuna nafasi ya chuki dhidi ya wayahudi nchini Ujerumani, bila kujali kama inachochewa kisiasa au kidini, kama inasababishwa na siasa za mrengo wa kulia au kushoto, kama imekulia Ujerumani kwa karne nyingi au inaingizwa nchini kutoka nje ya nchi.
Erdogan ameongeza kuwa iwapo Ujerumani itaungana na Uturuki katika kutoa wito wa kusitishwa mapigano Gaza, kuna nafasi ya hilo kufanyika.