Mawasiliano Gaza yapungua kwa siku ya pili mtawalia
17 Novemba 2023Volker Turk, Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza haja ya usitishwaji mapigano kwa misingi ya kibinadamu na haki za binadamu.
"Lazima kuwe na mwisho wa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, haswa dhidi ya watoto. Aina zote za adhabu ya pamoja lazima zifikie mwisho. Mateka wote lazima waachiliwe. Sheria ya kimataifa ya haki za kibinadamu na haki za binadamu lazima iheshimiwe mara moja na kikamilifu, ikijumuisha kanuni za umuhimu, utofautishaji, tahadhari na uwiano", alisema Turk.
Hayo yakijiri jeshi la Israel limesema kupitia ukurasa wa X kwamba limepeleka lita 4,000 za maji ya kunywa na mgao wa chakula 1,500 katika hospitali ya Shifa.
Jeshi la Israel laashiri kufanya mashambulizi Kusini mwa Gaza
Israel inaendeleza operesheni yake katika mji wa Gaza. Wanajeshi wake wamekuwa wakipekua hospitali kubwa zaidi ya mjini humo Al-Shifa, kutafuta kamandi ya kundi la Hamas ambayo jeshi lake lilidai iko chini ya jengo la hospitali hiyo.
Jeshi la Israel limeonyesha picha za kile lilichosema ni lango la handaki na silaha zilizopatikana kwenye lori ndani ya hospitali hiyo. Lakini bado hakuna ushahidi wa kuwepo kwa kamandi ambayo kundi la Hamas na wafanyakazi wa hospitali hiyo wamekanusha kuwepo.
Israel, Marekani na Umoja wa Ulaya huiita Hamas kama la kundi la kigaidi.