1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UhamiajiTunisia

Watoto 289 walikufa wakijaribu kuvuka bahari ya Mediterania

15 Julai 2023

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto UNICEF limesema kuwa watoto 289 wanaaminika kufariki katika nusu ya kwanza ya mwaka 2023 walipokuwa wakijaribu kuvuka bahari ya Mediterania kuelekea Ulaya.

https://p.dw.com/p/4TwNW
Italien Kalabrien Cutro | Bootsunglück mit vielen Toten
Picha: Alessandro Serranó/AGF/Avalon/Photoshot/picture alliance

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto UNICEF limesema kuwa watoto 289 wanaaminika kufariki katika nusu ya kwanza ya mwaka 2023 walipokuwa wakijaribu kuvuka bahari ya Mediterania kuelekea Ulaya.

UNICEF imeeleza kuwa idadi ya vifo hivyo ni mara mbili zaidi ya iliyorekodiwa katika miezi sita ya kwanza ya mwaka 2022.

Shirika hilo limehimiza kuwekwa kwa njia salama na za kisheria kwa watoto wanaojaribu kuingia Ulaya kwa ajili ya usalama wao.

Afisa wa UNICEF anayehusika na masuala ya uhamiaji Verena Knaus amesema idadi hiyo huenda ikawa kubwa zaidi maana kuna baadhi ya ajali za boti kwenye bahari ya Mediterania ambazo hazinakiliwi.

Soma pia: Watu 11,000 wakimbia makaazi yao kusini magharibi mwa Niger

Knaus ameongeza kuwa katika miezi sita ya kwanza ya mwaka huu, inakadiriwa kuwa watoto 11,600 walivuka bahari ya Mediterania- idadi hiyo ikiwa karibu mara mbili katika kipindi kama hicho mwaka uliopita.

"Vifo hivi vinaweza kuepukika kabisa," ameeleza Knaus.

Katika miezi mitatu ya kwanza ya mwaka 2023, watoto wapatao 3,300- asilimia 71 ya watoto wanaoingia Ulaya kupitia njia ya bahari ya Mediterania- walifanya safari hizo bila ya aidha ya kusindikizwa na mtu mzima ama walitenganishwa njiani.

Idadi hiyo ni mara tatu zaidi katika kipindi kama hicho mwaka jana.

Afisa huyo wa UNICEF amekiri kuwa watoto wengi walikuwa wakifanya safari hizo za hatari wakitumia muda mrefu wakati mwengine au hata miezi ili kufika katika pwani za Libya, Tunisia na mataifa ya Afrika Kaskazini.

Wengi wao walikuwa wakitokea Guinea, Senegal, Gambia, Syria na hata Afghanistan.

Soma pia: Mahakama UK yaukataa mpango wa serikali kupekela waomba hifadhi Rwanda 

Wakiwa njiani, wanaweka maisha yao hatarini na aghalabu hukabiliwa na visa vya unyanyasaji, ubakaji, biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu huku wasichana hasa wakiwa katika hatari kubwa zaidi.

UNICEF imesema kuwa safari ya boti kutoka Libya au Tunisia kuelekea Ulaya hugharimu takriban dola za Kimarekani 7,000.

"Hawa watoto wanapaswa kujua kwamba hawako pekee yao, viongozi wa dunia wanafaa kuchukua hatua za haraka kuokoa maisha ya watoto. Salamu za faraja pekee hazitoshi, wanapaswa kuchukua hatua madhubuti na kutafuta suluhu ya kadhia hii," amesema Knaus.