UNICEF: Ukeketaji wanawake waathiri wanawake milioni 230
8 Machi 2024Claudia Coppa, mwandishi mkuu wa ripoti hiyo ya UNICEF, iliyotolewa Alhamisi, siku moja kabla ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake, amesema takwimu hiyo ni ya juu mno kuwahi kushuhudiwa na kuongeza kuwa ni habari mbaya.
Juhudi za kukabiliana na ukeketaji wanawake zinapaswa kuimarishwa
Coppa amesema kuwa juhudi zinapaswa kuongezwa mara 27 zaidi ya kiwango cha sasa kutokomeza utaratibu huo wa ukeketaji wanawake kufikia mwaka 2030 kama ilivyoratibishwa katika agenda ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo Endelevu.
Kubadilisha desturi kutachukuwa muda
Coppa ameongeza kuwa ijapokuwa mitazamo inabadilika , ukeketaji wanawake umekuwa ukifanyika kwa miongo kadhaa sasa hivyo basi kubadilisha desturi za kijamii kuhusiana na utaratibu huo itachukuwa muda.
Soma pia:Kenya: Kampeni ya kukabiliana na ukeketaji wazinduliwa
Coppa pia amesema kuwa katika baadhi ya jamii kwa mfano, ukeketaji wanawake unachukuliwa kama utamaduni wa kudhibiti masuala mbali mbali yanayohusiana na hali ya kuwa mwanamke.
Ufaransa yapitisha sheria ya kuruhusu uaviaji mimba
Katika kura ya kihistoria siku ya Jumatatu, mabunge yote mawili ya Ufaransa yaliidhinisha uaviaji mimba kama haki ya kisheria , hatua iliyopokelewa kwa shangwe na watetezi wa haki za wanawake.
Hafla ya kushuhudia hatua hiyo kuwa ya kisheria imepangiwa leo ambayo ni Siku ya Kimataifa ya Wanawake, na inakuja mwaka mmoja baada ya Rais Macron kuahidi kuchukuwa hatua hiyo.
Hatua hiyo inaungwa mkono na raia wengi wa Ufaransa ijapokuwa kuna baadhi ya watu wanaoipinga.
Ufaransa yataka sheria ya uaviaji mimba itumike Ulaya
Siku ya Jumatano, msemaji wa serikali ya Ufaransa Prisca Thevenot, alisema kwamba Ufaransa lazima sasa itetee sheria hiyo hadi katika ngazi ya Umoja wa Ulaya.
Thevenot amesema kwamba mnamo mwaka 2022, Rais Macron alisema kuwa alitaka kuongeza haki hiyo ya uaviaji mimba katika mkataba wa haki za kimsingi za Umoja wa Ulaya.
Human Rights Watch yasema haki za wanawake zimekandamizwa
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, HRW limesema kuwa serikali nyingi zinazohofia mshikamano na hatua za pamoja za wanawake, zimekandamiza haki za kujieleza kwa wanawake kupitia vikwazo mbali mbali, kampeini za kuharibia sifa na mashtaka ya jinai.
HRW imetolea mfano mataifa kama vile Afghanistan na Iran, ambapo wanawake wanakamatwa na kuzuiwa kiholela na pia kulazimishwa kutoweka pamoja na kuteswa kutokana na harakati zao.
HRW yasema mitandao ya kijamii yachangia katika ukandamizaji wanawake
HRW imesema kuwa kampuni za mitandao ya kijamii, hazijachukuwa hatua za kutosha kuwalinda wanawake dhidi ya vurugu za mitandaoni hivyo basi kuchangia katika ukandamizaji wa uhuru wa wanawakekujieleza katika mitandao hiyo.
HRW imesema kuwa siku ya leo kuna mengi ya kusherehekewa na mengi ya kuomba na kuwataka wanawake kutumia haki yao ya kujielezea na kusikika.