Waafghani 1,000 wameuawa tangu Taliban ilipoingia mamlakani
28 Juni 2023Kulingana na ripoti mpya ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan UNAMA, tangu kundi la Taliban lilipoingia madarakani katikati ya Agosti 2021 hadi mwisho wa Mei, kulikuwa na wahanga 3,774 wa kiraia, wakiwemo 1,095 waliouawa katika vurugu nchini humo.
Idadi hiyo inalinganishwa na wahanga 8,820 wa kiraia, wakiwemo 3,035 waliouawa katika mwaka 2020 pekee.
Soma pia: UN yaionya Taliban kuhusu haki za wanawake na wasichana
Kulingana na ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa, robo tatu ya mashambulizi hayo tangu Taliban kuingia madarakani, yalitekelezwa kwa kutumia vifaa vya milipuko vilivyotengenezwa kienyeji katika maeneo yenye watu wengi, yakiwemo maeneo ya ibada, shule na masoko.
Miongoni mwa waliouawa ni wanawake 92 na watoto 287.
Takwimu hizo zinaonyesha ongezeko kubwa la madhara kwa raia yanayotokana na mashambulizi ya vilipuzi kwenye maeneo ya ibada - mengi yakiwa ya jamii ya Waislamu wachache wa madhehebu ya Kishia, ikilinganishwa na kipindi cha miaka mitatu kabla ya kuingia madarakani kwa Taliban.
Mashambulizi yanaripotiwa kufanywa na kundi la Dola la Kiislamu IS
Taarifa hiyo pia ilisema kuwa watu wasiopungua 95 waliuawa katika mashambulizi dhidi ya shule , taasisi za elimu na maeneo mengine ambayo yalilelenga zaidi jamii ya Kishia ya Hazara.
Taarifa hiyo imesema mashambulizi mengi yalifanywa na tawi la kundi linalojiita dola la kiislamu IS, linalojulikana kama dola la kiislamu katika jimbo la Khorasan, kundi la wanamgambo wa Kisunni ambalo ni mpinzani mkuu wa Taliban.
Fiona Frazer, mkuu wa huduma ya haki za binadamu katika ujumbe huo wa UNAMA, amesema mashambulizi hayo dhidi ya raia na mali zao hayafai na yanapaswa kukomeshwa mara moja.
Pia aliuhimiza uongozi wa Taliban kuzingatia wajibu wao wa kulinda haki ya maisha ya watu wa Afghanistan.
Hata hivyo, ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa imesema idadi kubwa ya vifo hivyo ilitokana na mashambulizi ambayo hakuna aliyedai kuhusika nayo ama ambayo ujumbe wa Umoja wa Mataifa haukuweza kuhusisha na kundi lolote. Ripoti hiyo haikutoa idadi ya vifo hivyo.
Soma pia: Mateso ya Taliban kwa wanawake ni uhalifu dhidi ya ubinadamu
Ripoti hiyo pia ilielezea wasiwasi kuhusu hatari ya mashambulizi ya kujitoa mhanga tangu Taliban ilipochukuwa uongozi huku mashambulizi machache yakisababisha vifo zaidi vya raia.
Katika kujibu, wizara ya mambo ya nje ya Afghanistan inayoongozwa na Taliban, imesema kwamba hali nchini humo imeimarika kwa hatua tangu Agosti mwaka 2021.
Taliban pia imesema kuwa usalama umehakikishwa kote nchini humo na kuongeza kuwa uongozi wake unazingatia usalama wa maeneo ya ibada na madhabahu matakatifu yanayojumuisha maeneo ya Kishia kuwa suala la kipaumbele.