UN yasema msaada usio na kikomo wahitajika Gaza
27 Oktoba 2023Kamishna mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi wa Kipalestina UNRWA, Philippe Lazzarini amesema watu wa Gaza wanakufa sio tu kutokana na mashambulizi ya mabomu, bali wengi watakufa kutokana na matokeo ya kuzingirwa kwa Ukanda wa Gaza huku huduma za msingi zikiathirika pakubwa na kukishuhudiwa uhaba wa dawa, chakula na maji. Aidha Lazzarini amesema mitaa ya Gaza sasa imejaa maji taka na kwamba hilo ni hatari:
"Gaza iko kwenye ukingo wa hatari kubwa ya kiafya, na hatari ya magonjwa inakaribia." Kinachohitajika ni mtiririko wa maana na usiokatizwa wa misaada. Na ili kufanikiwa hili, tunahitaji usitishaji mapigano kwa sababu za kibinadamu ili kuhakikisha msaada huu unawafikia wale wanaouhitaji."
Hata hivyo, misaada ya kibinaadamu imeendelea kuwasilishwa, ambapo hapo jana malori kumi na mawili zaidi yaliyosheheni maji ya kunywa, chakula na bidhaa nyingine yaliwasili Gaza. Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa, kabla ya shambulio la kigaidi la Hamas nchini Israel 7 Oktoba, takriban malori 500 ndiyo yaliyokuwa yakivuka mpaka kila siku kuingia huko Gaza.
Israel yaendeleza mashambulizi Gaza
Kulingana na wizara ya Afya inayodhibitiwa na kundi la Hamas, watu 481 wameuawa katika kipindi cha saa 24 zilizopita. Kwa mujibu wa mamlaka huko Gaza na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uratibu wa Masuala ya Kibinadamu (OCHA), hadi sasa jumla ya Wapalestina 7,028 wameuawa tangu kuanza kwa mzozo huu Oktoba 7 huku asilimia 66 kati yao wakiwa ni wanawake na watoto.
Soma pia:Ulaya yataka eneo salama la kibinaadamu kuundwa Gaza
OCHA imetoa pia tathmini ya uharibifu ambapo imesema asilimia 45 ya nyumba zote katika Ukanda wa Gaza zimeharibiwa ikiwa ni sawa na nyumba 150,000 ama zilizoharibiwa au kutoweza tena kukaliwa.
Jeshi la Israel limesema kundi la Hamas huficha zana zao za kijeshi katika majumba ya raia. Jeshi hilo limebainisha kwamba linajaribu kadri iwezekanavyo kuepusha majeruhi ya raia na kusisitiza kuwa hutoa onyo ya kuwataka raia kuondoka kabla ya mashambulizi ya roketi.
Kulingana na vyombo vya habari vya Urusi, Abou Hamid ambaye ni miongoni mwa viongozi wa kundi la Hamas walioko ziarani mjini Moscow, amesema mateka wa Israel kamwe hawatoachiwa huru hadi kutakapofikiwa makubaliano ya usitishwaji mapigano na kusisitiza kuwa mazingira tulivu yanahitajika ili kukamilisha zoezi hilo. Hapo jana kundi la Hamas lilisema karibu mateka 50 tayari wameuawa katika mashambulizi ya anga ya Israel.