UN yaidhinisha uondoaji wa vikosi vya AMISOM Somalia
3 Julai 2023Mnamo Aprili 2022, Baraza la Usalama liliidhinisha kubadilishwa kwa AMISOM, Ujumbe wa Umoja wa Afrika nchini Somalia, uliyoundwa mwaka 2007, na ATMIS (Ujumbe wa Mpito wa Afrika nchini Somalia), ambao pia unaongozwa na AU lakini kwa mamlaka iliyoimarishwa ya kupambana na wapiganaji wa itikadi kali wa kundi la Al-Shabaab.
Kikosi cha ATMIS, ambacho kilikuwa kimejumuisha zaidi ya askari 19,000 na maafisa wa polisi, kitalazimika kupunguzwa hadi sifuri mwishoni mwa 2024, na kuhamishwa taratibu kwa shughuli zake kwa vikosi vya Somalia.
Kwa mujibu wa maazimio ya awali ya Baraza la Usalama, ATMIS ilianza kuwaondoa wanajeshi 2,000 siku chache zilizopita, mchakato unaopaswa kukamilika mwishoni mwa Juni.
Uondoaji huo "unakaribia kukamilika," naibu balozi wa Somalia Mohamed Rabi Yusuf alisema Jumanne, akiongeza kwamba serikali yake itafanya "maandalizi ya lazima kwa uratibu na Umoja wa Afrika kwa awamu ya pili na kuwaondoa wanajeshi 3,000 wa ATMIS ifikapo Septemba."
Azimio la kuidhinisha ATMIS hadi mwisho wa 2023 lilipitishwa kwa kauli moja Jumanne, na kuweka kikomo kipya cha wanajeshi 14,626 kutoka Oktoba 1 hadi Desemba 31.
Soma pia: Al Shabab yadai imewauwa Wanajeshi 57 wa Kenya
Baraza pia lilisema "liko tayari kupitia tarakimu hizi" kwa kuzingatia matokeo ya tathmini ya kiufundi itakayotolewa na Somalia na AU ifikapo Septemba 15, haswa kutathmini awamu ya kwanza ya uondoaji huo na kutoa mpango na ratiba ya wazi kwa waliosalia.
Likibainisha "maendeleo" ya Somalia dhidi ya kundi tanzu la Al-Qaeda, azimio hilo linaonyesha "wasiwasi mkubwa kwamba kundi la kigaidi la Al-Shabaab linaendelea kuwa tishio kubwa kwa amani, usalama na utulivu wa Somalia na kanda."
"Hatupaswi kufanya haraka linapokuja suala la kuondoa ujumbe wa kulinda amani wa Afrika kutoka Somalia," Naibu Balozi wa Urusi Anna Evstigneeva alisema. "Kuunda ombwe la usalama hakukubaliki." Kutokana na hali hii, Somalia tena ilitoa wito wa kuondolewa kwa vikwazo vya silaha.
"Nusu marufuku ya silaha ya Umoja wa Mataifa kwa Somalia inazuia uwezo wa serikali ya shirikisho ya Somalia kutoa zana za kutosha kwa vikosi vyake vya usalama ili kukabiliana na tishio linaloendelea la Al-Shabaab," alisema Yusuf.
Mnamo Novemba, Baraza la Usalama lilirefusha vikwazo vya silaha vilivyowekwa tangu 1992. Vikwazo hivi havitumiki tena kwa utoaji wa silaha kwa ajili ya maendeleo ya vikosi vya usalama vya Somalia.
Hata hivyo, kamati ya Umoja wa Mataifa inayohusika na vikwazo lazima ipewe notisi ya uwasilishaji huo, na inaweza kupinga katika mazingira ya silaha nzito.
Chanzo: AFP