Uganda yathibitisha kuuawa wanajeshi wake 54 nchini Somalia.
4 Juni 2023Kundi la wapiganaji la Al-Shabaab nchini Somalia limedai kuhusika na mashambulio dhidi ya kituo cha vikosi vya Uganda nchini Somalia alfajiri ya tarehe 26 mwezi Mei. Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema wanajeshi wasiopungua 54 wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika waliuawa katika shambulizi hilo la wiki iliyopita.
Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (UPDF) limeirejesha kambi hiyo mikononi mwao kutoka kwa kundi hilo la Al Shabaab. Amewasifu askari wake kwa ujasiri walionoyesha na
Katika taarifa iliyochapishwa kwenye ukurasa wake rasmi wa mtandao wa Twitter, Museveni amesema miongoni mwa wanajeshi waliouawa ni kamanda.
Idadi hiyo ya vifo ni kubwa zaidi tangu vikosi vinavyoiunga mkono serikali vikiungwa na kikosi cha Umoja wa Afrika, maarufu kama ATMIS, vilipoanzisha mashambulizi Agosti mwaka jana dhidi ya Al-Shabaab.
Walinda amani hao 54 wa Uganda walikufa wakati wanamgambo walipozingira kambi ya Umoja wa Afrika nchini Somalia.
Washambuliaji hao walitumia gari lililokuwa na vilipuzi na kuingia katika kambi ya Bulo Marer, iliyo umbali wa kilomita 130 kusini magharibi mwa mji mkuu wa Somalia, Mogadishu. Hali hiyo ilisababisha makabiliano ya risasi kati ya wanajeshi na wapiganaji hao kwa mujibu wa wakazi wa eneo hilo na kamanda wa jeshi la Somalia.
Kundi la Al Shabaab, limekuwa linaendeleza mashambulizi nchini Somali tangu mwaka 2006 kwa lengo la kuchukua nafasi ya serikali ya Somalia inayoungwa mkono na nchi za Magharibi. Al Shabaab inataka kuweka utawala wake wenye msingi wa kidini unaoelemea sheria kali.
Vyanzo:AFP/RTRE