UN yahimiza hatua za kupambana na chuki za kidini
12 Julai 2023Pendekezo la azimio hilo liliwasilishwa na Pakistan baada ya kisa cha kuchomwa hadharani kwa kitabu kitakatifu kwa Waislamu cha Qur'an kilichotokea hivi karibuni nchini Sweden na kuzusha hasira miongoni mwa waumini wa dini hiyo duniani.
Soma pia: Iran yasitisha kumpeleka balozi wake nchini Sweden kupinga kitendo cha kuchomwa kwa Quran
Kwenye kikao cha baraza hilo kinachoendelea mjini Geneva, mataifa 28 yamepiga kura za ndiyo kuidhinisha azimio hilo huku nchi 12 zikilipinga na nyingine 7 zikijizuia kupiga kura.
Chini ya azimio hilo, mataifa ulimwenguni yanatolewa mwito wa kuzipitia upya sheria na kuziba mianya inayoweka vizingiti vya kushughulikiwa kwa matendo yanayochochea chuki za kidini.
Hata hivyo, azimio hilo linapingwa vikali na mataifa mengi ya Magharibi yakiongozwa na Marekani yanayosema linatishia uhuru wa watu kujieleza.