Watu milioni 13 wakabiliwa na njaa katika Pembe ya Afrika
8 Februari 2022Shirika hilo la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limekadiria idadi hiyo ya watu wapatao milioni 13 wanaokabiliwa na janga la njaa kutokana na ukame katika nchi za Kenya, Somalia na Ethiopia. WFP imesema eneo la Pembe ya Afrika limekumbwa na ukame mbaya zaidi kuwahi kutokea katika kipindi cha miongo kadhaa. Mkurugenzi wa WFP Kanda ya Afrika Mashariki Michael Dunford kutoka Nairobi amesema hali ya ukame inaziathiri jamii za wafugaji na wakulima kote katika nchi hizo.
Amesema baada ya kuwepo misimu mitatu ya ukosefu wa mvua katika Pembe ya Afrika, eneo hilo linakabiliwa na ukame mkubwa unaowaathiri watu takriban milioni 13 na maeneo ya kusini mwa Ethiopia, kaskazini mwa Kenya na Somalia yameathiriwa sana. Dunford amsema, mifugo inakufa, mazao yanapungua na hali hiyo inasababisha idadi kubwa ya watu kulazimika kuyahama makazi yao.
Ripoti ya WFP imeeleza kwamba viwango vya utapiamlo ni vya juu katika kanda hiyo ya Afrika Mashariki. WFP imesema hali hiyo ya ukame inasababisha kuongezeka kwa migogoro ya jamii. Utabiri wa hali hewa unaashiria hali mbaya zaidi ya ukame kutokana na mvua chache za chini ya wastani katika miezi ijayo.
Kwa upande wake shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia watoto UNICEF mapema mwezi huu wa Februari lilisema zaidi ya watu milioni 6 nchini Ethiopia watahitaji msaada wa dharura ifikapo katikati ya mwezi Machi. Katika nchi jirani ya Somalia, zaidi ya watu milioni 7 wanahitaji msaada wa haraka, kulingana na Muungano wa mashirika yasiyo ya kiserikali nchini humo. Shirika la WFP limetoa wito wa msaada wa haraka ili kuepusha maafa makubwa yanayoweza kusababisha mgogoro wa kibinadamu.
WFP imesema inahitaji kiasi cha dola milioni 327 kushughulikia mahitaji ya dharura ya watu milioni 4.5 katika muda wa miezi sita ijayo ili kuzisaidia jamii ziweze kustahimili majanga makubwa yanayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa.
Vyanzo: AP/AFP