UN: Waasi wa Houthi kutowatumia tena watoto kama wanajeshi
19 Aprili 2022Umoja wa Mataifa umesema waasi hao wametia saini kile kilichoelezewa kama "mpango" wa kufikisha mwisho na kuzuia usajili na kutumiwa kwa watoto katika mapigano, kuuwawa au kujeruhiwa kwao na kushambuliwa kwa shule na hospitali.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema waasi hao wamedhamiria kuwatambua watoto miongoni mwao na kuwaachia huru ndani ya kipindi cha miezi sita ijayo.
Mmoja wa wanadiplomasia wakuu wa Wahouthi Abdul Eluh Hajaar ndiye aliyetia saini makubaliano hayo.
Serikali ya Yemen nayo yatia saini makubaliano
Philippe Duamelle ni mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia watoto UNICEF.
"Kwa hiyo tunatazamia kushirikiana na pande zote zinazohusika na mamlaka mjini Sanaa na utekelezaji kamili wa mpango uliotiwa saini. Na tunatazamia kuendelea kufanya kazi na pande zote ili kuboresha usalama kwa watoto nchini Yemen na kumaliza ukiukaji mkubwa wa haki zao," alisema Duamelle.
Umoja wa Mataifa umesema serikali ya Yemen inayotambulika kimataifa na ambayo inafanya kazi uhamishoni, imedhamiria hayo pia katika nyaraka ilizotia saini tangu mwaka 2014.
Umoja wa Mataifa unasema imethibitishwa kwamba watoto 3,500 wamesajiliwa na kupelekwa katika uwanja wa mapambano katika vita yva wenyewe kwa wenyewe nchini Yemen. Lakini afisa mmoja mwandamizi wa kijeshi wa waasi wa Houthi mwaka 2018 aliliambia shirika la habari la Associated Press kwamba, walikuwa wamewasajili watoto 18,000 katika jeshi lao kufikia mwaka huo. Wanajeshi wa zamani watoto nao walisema hata wavulana walio na umri wa hadi miaka 10 walikuwa wakisajiliwa.
Rais Abed Rabbo Mansour Hadi ajiuzulu
Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kwamba zaidi ya watoto 10,200 wameuwawa au kujeruhiwa katika vita hivyo ila haibainiki ni wangapi miongoni walikuwa wanajeshi.
Pande zinazohasimiana nchini Yemen mapema mwezi huu zilikubaliana kusitisha mapigano kote nchini humo kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka sita. Makubaliano hayo ya kuweka chini silaha yalikuwa yananuiwa kuanza katika mwezi wa Ramadhani na uliibua matumaini ya kupatikana kwa amani.
Rais wa Yemen Abed Rabbo Mansour Hadi alijiuzulu wiki iliyopita na kusema baraza jipya la rais litaiendesha serikali hiyo na kuongoza mazungumzo na Wahouthi.
Chanzo: APE