Dola bilioni 4.27 zinahitajika kwa ajili ya Yemen
16 Machi 2022Hafla hiyo ya uchangishaji fedha inafanyika Jumatano kwa njia ya video na imeandaliwa kwa ushirikiano wa Sweden na Uswisi. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres na nyota wa filamu kutoka Hollywood, Angelina Jolie, watawahutubia wafadhili kuhusu mahitaji makubwa ya nchi hiyo masikini zaidi katika mataifa ya Kiarabu.
Mzozo wa Yemen katikati ya uvamizi wa Urusi Ukraine
Mkutano huo unafanyika wakati ambapo ulimwengu umegubikwa na vita nchini Ukraine, ambavyo vimefunika mizozo mingine ya kiutu duniani kote tangu Urusi ilipoivamia nchi hiyo Februari 24 na kuzusha wasiwasi kwamba hali ya Yemen inaweza kusahaulika. Zaidi ya watu milioni tatu wamekimbia Ukraine, idadi inayoelezwa kuwa kubwa zaidi barani Ulaya tangu Vita Kuu ya Pili ya Dunia.
Akizungumza kabla ya mkutano huo, Balozi wa Sweden, Carl Skau amewasihi wafadhili kuizingatia Yemen. Skau amesema ingawa Ukraine inaeleweka na kwa haki inahitaji msaada wa haraka zaidi, ombi lao ni kutosahaulika kwa mizozo mingine.
Bei za mahitaji muhimu kama vile chakula na hasa gharama ya nafaka inatarajiwa kuongezeka nchini Yemen. Kwa mujibu wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, asilimia 22 ya ngano inayotumika Yemen inatoka Ukraine.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO wiki hii limeripoti kuwa watoto milioni 2.2 wana utapiamlo mbaya nchini Yemen na nusu milioni wako katika hali mbaya inayotishia maisha yao.
Mkutano wa mwaka uliopita ulichangisha tu dola bilioni 1.7 kwa ajili ya Yemen kati ya dola bilioni 3.85 ambazo Umoja wa Mataifa uliomba, wakati ambapo janga la virusi vya corona na matokeo yake mabaya yaliuathiri uchumi kote duniani. Guterres aliyaelezea matokeo ya mwaka 2021 kama ya kukatisha tamaa.
Mzozo wa Yemen ulioanza mwaka 2014, umesababisha mauaji ya zaidi ya watu 150,000, wakiwemo raia 14,500. Vita hivyo pia vimesababisha mzozo mbaya zaidi wa kibinaadamu ulimwenguni, na kuwaacha mamilioni wakiwa hawana chakula na uhaba wa huduma za afya na kutumbukiza nchi hiyo kwenye ukingo wa baa la njaa.
Watu wengi wanaishi maeneo ya Wahouthi
Idadi kubwa ya watu wapatao milioni 32 wa Yemen wanaishi kwenye maeneo yanayodhibitiwa na waasi wa Kihouthi. Waasi hao kwa miaka mingi wamehusishwa na wizi wa misaada na kuizuia misaada hiyo.
Mapema mwaka huu, wataalamu wa Umoja wa Mataifa waliripoti kwamba waasi walizinyima misaada ya kiutu familia ambazo watoto wao walishiriki katika mapigano au kwa walimu kwa misingi kwamba walifundisha mtaala kuhusu Wahouthi.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu misaada ya kiutu, OCHA imeonya kuwa jumla ya watu milioni 19 wanatarajiwa kukabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula ifikapo nusu ya pili ya mwaka huu, ongezeko la karibu asilimia 20 ikilinganishwa na miezi sita ya kwanza ya mwaka 2021. OCHA imesema kati yao, watu 161,000 wana uwezekano wa kukumbwa na baa la njaa kwa mwaka huu wa 2022.
(AP, DPA, Reuters)