1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Uganda lazima ifute sheria yake mpya ya kupinga ushoga

Hawa Bihoga
27 Julai 2023

Ukiukaji wa haki za binadamu ikiwa ni pamoja na mauaji ya kiholela nchini Uganda katika miaka ya hivi karibuni umeibua wasiwasi kwa jopo la wataalamu wa Umoja wa Mataifa huku wakitaka kufutwa sheria inayopinga ushoga.

https://p.dw.com/p/4USSn
UN Sondersitzung Sudan
Picha: FABRICE COFFRINI/AFP/Getty Images

Kamati ya Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu katika taarifa yake ilioitoa leo Jumatano, imeitaka pia mamlaka katika taifahilo la Afrika Mashariki kufuta sheria yake ilioiweka hivi karibuni inayotoa adhabu ya kifo, kwa baadhi ya watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja.

Kamati pia ilielekeza ripoti za kukamatwa na kuwekwa kizuizini kiholela na polisi na vikosi vya usalama kuwalenga wapinzani wa kisiasa, waandishi wa habari, wanasheria, watetezi wa haki za binadamu, wafanyabiashara ya ngono, na watu wanaotetea na kushiriki mapenzi ya jinsia moja.

Katika ripoti hiyo ambayo ni mapitio ya kwanza kwa Uganda tangu mwaka 2004, imeonesha pia vikosi vya usalama nchini humo vinakabiliwa na madai yanayoongezeka ya ukatili katika kuwakabili wanaodhaniwa kuwa wapinzani wa serikali ya Rais Yoweri Museveni, mshirika wa Marekani ambaye amekuwa madarakani tangu 1986.

Jopo hilo la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu limehimiza kwamba kuna umuhimu wa kuangaliwa upya kesi za mauaji ya kiholela na wahalifu "waadhibiwe."

Soma pia:Museveni akaidi miito ya kumtaka afute sheria dhidi ya ushoga

Chama cha upinzani cha National Unity Platform kimeongoza wito kwa rais Museveni na baadhi ya maafisa wake wa usalama watakabiliwa na mashtaka ya uhalifu katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC.

Hata hivyo rais Museveni amelaani baadhi ya maafisa wa usalama kwa kutumia nguvu kupita kiasi wanaposhughulika na raia, wakosoaji wake wanasema anapaswa kuwajibika kwa unyanyasaji uliofanywa chini ya uangalizi wake.

Sheria ya kupinga ushoga yajadiliwa na jopo

Sheria mpya inayowalenga wapenzi wa jinsia moja imeiweka Uganda katika hali mbaya zaidi kwenye uga wa kimataifa.

Yoweri Musevini to sign anti-LGBT law
Rais wa Uganda Yoweri MuseveniPicha: ABUBAKER LUBOWA/REUTERS

Sheria hiyo inayotetewa na rais Museveni, inaungwa mkono kwa asilimia kubwa na wakaazi wa taifa hilo, huku imekosolewa na wanaharakati wa haki za binadamu, kadhalika na wafadhili wa kiuchumi wa taifa hilo linaloendelea, ikiwemo Benki ya Dunia.

Soma pia:Biden akosoa sheria ya Uganda dhidi ya wapenzi wa jinsia moja na kuhimiza kufutwa

Marekani imeonya madhara makubwa ya kiuchumi juu ya sheria iliyoelezwa na shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International kama ya "kibabe kupindukia."

Jose Manuel Santos Pais, mjumbe wa kamati ya hiyo ya Umoja wa Mataifa alisema "hawaelewi mantiki" najumuiya ya kimataifa imeshtushwa na sheria hiyo.

Mapenzi ya jinsia moja yameharamishwa kisheria katika mataifa 30 barani Afrika, huku baadhi ya waafrika wakiamini kwamba tabia hizo zimeingizwa kutoka mataifa ya nje na si mwelekeo wa jadi wa kijinsia.

Museveni aitetea sheria ya kupinga ushoga